Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameeleza jinsi matapeli wa ardhi wanavyoshirikiana na baadhi ya maafisa ardhi hasa wa Halmashauri za Manispaa na Jiji kutekeleza utapeli wa ardhi kwa kutumia barua bandia za toleo (ofa).
Lukuvi ameeleza hayo leo wakati akihojiwa katika kipindi cha Kumekucha kinachorushwa na kituo cha runinga cha ITV.
Amesema asilimia 60 ya kesi za migogoro ya ardhi inayofika wizarani kwake, chanzo ni muingiliano wa umiliki ardhi ambapo kiwanja kimoja kinamilikiwa na zaidi ya mtu mmoja.
“Mtu akinunua ardhi hupewa karatasi za ofa ambazo hivi sasa zilizojaa ni feki, lakini wapo wajanja na matapeli wanatumia ofa hizo kudhurumu viwanja vilivyo wazi. Mfano wakiona kiwanja kipo wazi wanakwenda katika halmashauri wanashirikiana na baadhi ya maafisa ardhi wasio waaminifu, wanauliza namba ya ploti ya kiwanja husika na anayemiliki,” amesema.
Ameongeza kuwa” Wakishajua namba na mmiliki wa kiwanja huiondoa ofa halali katika faili kisha afisa ardhi anaiweka feki, siku mmiliki halali akienda kuulizia kiwanja chake katika halmashauri anakuta ofa yake haipo ipo ya mtu mwingine ambaye ameghushi tarehe ya barua ya ofa.”
Amesema matapeli wa ardhi huyafahamu maeneo yaliyowazi na kwamba asilimia kubwa hushughulika na yale ambayo wamiliki wake wamefariki dunia.
“Hawa matapeli huyajua maeneo vizuri, na wanachokifanya ni kutengeneza ofa feki kisha kuziweka katika faili za halmashauri, ukienda mmiliki halali unaambiwa ni tapeli kwa kuwa barua yako haiko katika faili,” amesema na kuongeza.
“Matapeli wanaishi mjini kwa kutengeneza ofa bandia, wastaafu,yatima na wajane wanalizwa kila siku,” amesema.
Ametoa agizo kwa maafisa ardhi wa kanda kutotoa huduma wala kushugulika na barua za ofa kwa sababu baadhi yao ndio wanaobadilisha ofa halali za watu.
“Maafisa ardhi wa kanda zote wasipokee wala kutoa huduma kwa mtu mwenye ofs sababu baadhi yao ndio wanaosababisha utapeli wa ardhi, wenye karatasi za ofa wazilete kwa kamishna ardhi wa mkoa sababu majalada yote halali na halisi yapo kwake hivyo hakuna mazingira ya utapeli,” amesema.