Jumapili, 9 Oktoba 2016

MWENGE WA UHURU WAANZA MBIO ZAKE MKOANI SIMIYU

Posted byEsta Malibiche on Oct9.2016 in  

 Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (kulia) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack  (kushoto) katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa ukitokea Kishapu Mkoani Shinyanga.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016, Ndg. George Mbijima akivikwa skafu na Vijana wa Skauti wa Wilaya ya Maswa kabla ya kupokelelewa na Viongozi wa Mkoa Simiyu, akitokea mkoani Shinyanga
 Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akimpokea Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016, Ndg. George Mbijima.
 Mkimbiza Mwenge Kitaifa kutoka Mkoa wa Simiyu, James Munguji akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa mapokezi ya mwenge wa Uhuru Mkoani Simiyu yaliyofanyika katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa.
 Baadhi ya Wakimbiza Mwenge Kitaifa wakisalimiana na viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa mapokezi ya mwenge wa Uhuru Mkoani Simiyu yaliyofanyika katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa.
 Mkimbiza Mwenge Kitaifa kutoka Mkoa wa Simiyu, James Munguji akisalimiana na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakati wa mapokezi ya mwenge wa Uhuru Mkoani Simiyu yaliyofanyika katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa.
 Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka akisoma taarifa ya Mkoa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016, Ndg. George Mbijima katika kijiji cha Wigelekelo wilayani Maswa mara baada ya kupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoani Shinyanga.

 Baadhi ya Viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakiwa tayari kushika Mwenge wa Uhuru mara baada ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru kutoka Shinyanga.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akimkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe.
Baadhi ya wasanii wa Ngoma ya Wagoyangi kutoka Maswa wakitoa burudani kwa kucheza ngoma wakiwa na nyoka aina ya chatu, mbele ya wananchi wa Wilaya hiyo waliofika katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika kijiji cha Wigelekelo
Na Stella Kalinga Simiyu

Mwenge wa Uhuru umepokelewa  ukitokea mkoani Shinyanga na kuanza mbio zake  mkoani Simiyu,  mkoa ambao kwa mujibu wa ratiba ni mwenyeji wa kilele chake kitaifa tarehe 14 Oktoba  mwaka 2016

Akitoa taarifa ya mkoa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 , George Mbijima Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka , amesema Mkoa huo unatekeleza kwa vitendo Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016 inayosema “Vijana ni nguvu kazi ya Taifa, Washirikishwe na kuwezeshwa’’ kwa kuwawezesha vijana wote kutekeleza miradi ya maendeleo  kupitia kauli mbiu ya Mkoa wa Simiyu ya “Wilaya moja Bidhaa moja”.


Mtaka amesema Mkoa umewahamasisha vijana kujiunga katika vikundi na kuwapatia mitaji katika kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuwa nchi ya Viwanda.

“Utekelezaji umeanza na Mkoa wa Simiyu tumejichagua kuwa mkoa wa utekelezaji, Utekelezaji huo upo ambapo Wilaya ya Maswa ‘kwenye wilaya moja bidhaa moja’ inazalisha chaki na Meatu inazalisha maziwa”, alisema Mtaka.

Aidha, Mtaka amesema kiwanda cha kuzalisha chaki cha Wilaya ya Maswa kitafunguliwa rasmi na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,Vijana, Ajira,Kazi na Wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), tarehe 10/10/2016  ambapo pia tarehe 11/10/2016 atafungua Kiwanda cha kusindika maziwa Meatu.

Aidha kuhusu ujumbe wa kudumu wa Mbio za Mwenge ; Serikali Mkoani Simiyu kwa kushirikiana na wadau wengine katika kupambana na madawa ya kulevya chini ya kaulimbiu ya “Tujenge jamii maisha na utu wetu;bila dawa za kulevya”  imeendelea kutoa elimu na kuchukua hatua kwa wasambazaji na watumiaji wa dawa za kulevya.

Katika Mapambano dhidi ya UKIMWI chini ya kauli mbiu “Tanzania bila maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na UKIMWI; Inawezekana” Mtaka  amesema mkoa unaendelea kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi kupima kwa hiari virusi vya Ukimwi ili waweze kutambua hali zao na kujilinda na maambukizi mapya, kuachana na unyanyapaa na kuzuia vifo.

Kuhusu mapambano dhidi rushwa chini ya kauli mbiu “Timiza wajibu wako; kata mnyororo wa rushwa” Mtaka amesema TAKUKURU kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa inaendelea kuwachukulia hatua wote wanaobainika kutoa na kupokea rushwa  na kutoa elimu kwa wananchi juu ya mapambano dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuelimisha kupitia klabu za wapinga rushwa mashuleni.

Sanjari na hilo Mtaka pia amesema Mkoa wa Simiyu unaendelea kupambana na Malaria chini ya Kauli mbiu “Wekeza katika Maisha ya baadaye; Tokomeza Malaria” kwa kuwahamasisha wananchi kutumia vyandarua, kuua mazalia ya mbu na kwenda katika vituo vya kutolea huduma za afya pindi wanapoona dalili za ugunjwa wa malaria.

Mhe. Anthony Mtaka amesema Mwenge wa Uhuru  ukiwa mkoani humo utapita katika Halmashauri sita (6) ukianzia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Meatu, Itilima, Busega, Bariadi na Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuona miradi minne (4),  kufungua miradi tisa (9), kuweka jiwe la msingi miradi sita(06) na kuzindua miradi 11 ya maendeleo katika sekta ya Afya, elimu, maji, kilimo, barabara, sekta binafsi na utawala bora ambayo kwa ujumla wake ina thamani ya zaidi ya bilioni 12.

0 maoni:

Chapisha Maoni