Posted by Esta Malibiche on Oct 4.2016 in NEWS
Hussein Makame, NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
imeandaa programu ya kutoa elimu ya mpiga kura katika vyuo vikuu nchini
ili kutoa fursa kwa wanavyuo kufahamu taratibu na Sheria zinazoongoza
uchaguzi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani, wakati akitoa tathmini ya
utekelezaji wa mkakati wa kutoa elimu ya mpiga kura nchini juzi jijini
Dar es Salaam jijini.
Alisema program hiyo itaanza kwa
kutoa elimu hiyo kwenye Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na baadaye kutoa elimu hiyo kwenye vyuo vingine nchini.
Mkurugenzi Kailima alieleza
programu hiyo kufafanua mikakati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kuhakikisha kuwa inatoa elimu ya mpiga kura kwa makundi mbalimbali
nchini ambayo kwa sasa inatolewa kwa wanafunzi wa shule za Sekondari
nchini.
“Lakini niseme vyuo vikuu
hatujavisahau kwa sababu tuna program hivi sasa kwamba tumepanga
tutakapokwenda vyuo vikuu, tutakwenda Chuo Kikuu cha Dodoma na chuo
kingine” alisema Bw. Kailima na kuongeza kuwa:
“Lakini tuna mpango wa kwenda
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vyuo vingine vyote tuzungumze nao, labda
niseme hapa kwamba hatwendi kuzungumza kuhusu uhalali wa katiba au
sheria zilizopo”
“Tunakwenda kuzungumza katiba ya
sasa inasemaje kuhusu taratibu za uchaguzi na utaratibu mzima na mfumo
wake ukoje, tunakwenda kuzungumza Sheria za sasa za Uchaguzi”
Bw. Kailima aliweka wazi kuwa
asingependa mikutano hiyo na vyuo vikuu kujadili kuhusu katiba bali
kuzungumzia Sheria zinazoiongoza tume kusimamia na kuratibu uchaguzi.
“Wewe ukiwa na hoja yako ya
katiba sio hii, hiyo ina jukwaa lingine watakuja wenye jukwaa lao
kuzungumzia suala hilo lakini sisi tunakuja kukwambia Sheria inasema
Tume isimamie na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura kwa ajili ya
uchaguzi wa Rais na wabunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”
alisema.
Alieleza kuwa Tume iliona umuhimu
wa kuanza kutoa elimu hiyo kwa ngazi ya sekondari ili kuwawezesha
wanafunzi wa ngazi hiyo kupata elimu ya mpiga kura mapema na kuepusha
vurugu zinazotokana na kukosekana kwa uelewa wa taratibu za uchaguzi.
“Unajua haya mambo kama
hamyazungumzi mapema ndio baadaye mnakuja kuyaona ni mageni, yanaleta
vurugu watu wanakatana mapanga lakini ikiwa ni kitu cha kawaida na
kinazunguzika vurugu zinakwisha” alifafanua Bw. Kailima.
Aliongeza kuwa wanafunzi wa shule
za sekondari ndio wagombea wa Urais na ubunge watarajiwa na ni
wenyeviti, makatibu na wajumbe wa vyama vya siasa watarajiwa na wakipata
elimu mapema itawajenga kujua Sheria ya Uchaguzi.
“Yule wa chuo kikuu tayari ni
mjumbe wa chama fulani, mwingine tayari ni mgombea, ueleweshaji wake
utakuwa sio mgumu kuliko yule wa shule ya sekondari” alisema.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi mbali
na kutoa elimu ya mpiga kura kwa wanafunzi wa shule za Sekondari nchini,
imepanga kuanzisha klabu za uchaguzi katika shule hizo ili kukuza
uelewa wa masuala mbalimbali ya uchaguzi kwa wanafunzi wa ngazi hiyo.
Sanjari na kutoa elimu hiyo kwa shule za sekondari, NEC pia
inashiriki katika maonesho na mikutano mbalimbali nchini ili kukutana na
wananchi ana kwa ana na kuwapa elimu hiyo.
0 maoni:
Chapisha Maoni