Jumanne, 4 Oktoba 2016

CHAMA CHA WATU WENYE UALIBINO MKOANI MWANZA CHATOA KILIO CHAKE KWA RAIS MAGUFULI.

Posted by Esta Malibiche on Oct4.2016 in NEWS

magufuli
Na BMG Chama cha watu wenye ualibino mkoani Mwanza, kimemuomba Rais John Pombe Magufuli, kukemea vikali vitendo vya ukatili ikiwemo kutekwa na kuuawa kwa watu hao kama anavyokemea masuala ya rushwa na ufisadi kwenye mikutano yake mbalimbali.
 
Mwenyekiti wa chama hicho, Alfred Kapole, ametoa ombi hilo Jijini Mwanza wakati
akizungumzia juhudi zinazofanywa na chama hicho ili kuhakikisha vitendo vya utekaji, ukataji viungo pamoja na mauaji kwa watu wenye ualibino nchini vinatokomezwa.
 
Amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kushirikiana na wanajamii katika kutokomeza vitendo hivyo, bado watu wenye ualibino nchini wanaishi kwa wasiwasi mkubwa kwani wamekuwa wakiwindwa na baadhi ya watu wenye imani potofu za kishirikina hivyo Rais Magufuli anapaswa kukemea vikali hali hiyo.
 
Mkoa wa Mwanza ni miongoni mwa mikoa yenye rekodi zisizoridhisha za matukio ya kutekwa, kukatwa viungo na kuuawa kwa watu wenye ualibino hapa nchini ambapo kesi tatu kati ya kesi 27 zilizoripotiwa mahakamani zimetolewa hukumu yake na wahusika kuhukumiwa adhabu ya kunyongwa.

0 maoni:

Chapisha Maoni