Jumatatu, 4 Aprili 2016

SERIKALI YA KATA YA MBALAMAZIWA YAANZA VITA DHIDI YA UGONJWA WA KIPINDUPINDU WASIO NA VYOO WAPIGWA FAINI ...

...


 
                                           Mkuu  wa mkoa wa Iringa Bi Amina Masenza 
.............................................................................................................................................................
WAKATI baadhi ya wilaya  za mkoa  wa Iringa  ikiwemo Iringa  vijijini na  Kilolo zimekumbwa na  ugonjwa  wa  kipindupindu kwa mwaka  huu kutokana na uchafu katika maeneo hayo ,serikali ya kata ya  Mbalamaziwa  wilaya ya Mufindi  mkoani hapa  imeanza oparesheni ya  kuwasaka  wananchi wasio  kuwa na vyoo bora na kuwatoza faini ya  uchafu.

Afisa  mtendaji  wa kata ya Mbalamaziwa  Bi Eliza Ngwaeje aliueleza  mtandao  huu wa matukiodaima leo  kuwa zoezi hilo ambalo  limeanza kuzaa matunda  katika  baadhi ya  vijiji  kwa  wananchi ambao  hawakuwa na  vyoo bora  kujenga  vyoo  hivyo ama  kuziweka vyoo vyao katika hali ya  usafi  zaidi tayari limeanza katika vijiji  vitano  kati ya sita   vilivyopo katika  kata  hiyo.

Alisema  kuwa  toka  kamati ya afya  ya kata  hiyo imeanza kutekeleza zoezi  hilo wananchi  wa  kata   hiyo wameonyesha  mwitikio mkubwa wa  kutekeleza agizo hilo la usafi ambalo mara kadhaa  mkuu  wa mkoa  wa Iringa Bi Amina Masenza  amekuwa akihimiza wananchi  kuwa na vyoo  bora piakuzingatia kanuni  za afya kwa kuweka mazingira   safi .

Bi Ngwaeje  alivitaja  vijiji ambavyo  wananchi  wameonyesha   kutekeleza agizo   hilo la usafi  kuwa ni pamoja na  Kitelewasi , Idetero, Maguvani,Ukemele na kwa  kiasi kijiji  cha Mbalamaziwa  na  kuwa kijiji  cha Nyanyembe hadi  sasa bado  hawajakifikia  na  kipo katika  ratiba  ya   kutembelewa kwa ajili ya ukaguzi  huo  wa  vyoo  bora na usafi.

" Tumekuwa na  changamoto  kubwa ya  utekelezaji  wa agizo   hilo kutoka kwa baadhi ya kaya  ambazo  ndugu  zao  wapo nje ya  mkoa  wa Iringa ambao  wamekuwa wakiwazuia ndugu   zao kutekeleza  agizo   hilo la  usafi na hata  kufika  kijijini  kuitisha mkutano wa  kuwazuia  ndugu  zao hao  kuwa na vyoo safi na bora....kweli  kama  viongozi  tunafanya kazi katika mazingira  magumu  sana katika  kutekeleza agizo hili la usafi hasa  kijiji  cha Mbalamaziwa ambao  hawataki kutii agizo hili"

Hata   hivyo  alisema  kuwa kisheria  kwa mujibu  wa sheria  za wizara  ya afya katika  wilaya ya  Mufindi adhabu  kwa  wasio  na  vyoo  bora na wanaopatikana na kosa la  uchafu ni kati ya Tsh 50,000 hadi 200,000 ila  kutokana na waanchi  hao  kukubali  kosa na  kutekeleza agizo la usafi kwa  wakati wamekuwa  wakiishia kuwatoza faini kati ya 30,000 hadi 50,0000 fedha ambazo  huingizwa katika  miradi ya  kimaendeleo katika kata   hiyo.

Afisa  mtendaji   huyo aliwataka  wakazi  wa Mbalamaziwa ambao wanaishi nje ya  mkoa  wa Iringa  kuacha  kuingilia utendaji  wa  serikali ya kata  katika  kusimamia usafi kwa  wananchi  wa kata   hiyo kwani madhara ya  kipindupindu yakitokea ambao wataathirika  ni  ndugu  zao ambao  wanaishi kijijini na  sio  wao  waliopo  mijini na  wao kama  viongozi  hawatarudi nyuma katika  kusimamia suala  zima  la usafi kwenye kata   hiyo.

0 maoni:

Chapisha Maoni