……………………………………………………………………………………………………
Na Ramadhani Ali/MAELEZO ZANZIBAR
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya
Zanzibar Dkt. Muh’d Dahoma amesema ili ugonjwa wa Kipindupindu umalizike
inategemea zaidi maamuzi ya familia na jamii kwa jumla kukubali
kubadilika.
Amesema desturi potofu na tabia za wananchi zinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maambukizi ya kipindupindu nchini.
Akifungua mafunzo ya siku moja kwa
waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa kipindupindu yaliyofanyika Wizara
ya Afya Mnazimmoja, Dkt. Dahoma amewataka waandishi wa habari kutoa
elimu zaidi kwa jamii ili wajue sababu zinazopelekea kuongezeka
ugonjwa huo na njia za kujikinga.
Amesema bado wananchi wanakuwa
wagumu kubadili mfumo wao wa maisha licha ya juhudi zinazochukuliwa na
Jumuiya za kimataifa, taasisi za Serikali na binafsi pamoja na vyombo
vya habari.
‘’Bado watu wanaishi katika
mazingira machafu, wengine hawana vyoo na wapo hawataki kuyatibu maji
ya kunywa, mambo yanayochangia mambukizi ya kipindupindu,’’ alisisitiza
Dkt. Dahoma.
Ameishauri jamii kuwa tayari
kubadilika baada ya kupata elimu ya maradhi ya kipindupindu ili
kupunguza vifo vinavyotokana na maradhi hayo.
Akitoa takwimu ya maradhi ya
kipindupindu tokea yalipoanza mwezi Septemba mwaka jana, amesema
wananchi 3,700 wameugua maradhi hayo na 46 kati yao wamefariki na
Wilya ya Magharibi inaongoza kwa kutoa wagonjwa wengi zaidi.
Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia
katika afya na mawasiliano kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Nd. Salum
Aboubakar amewashauri wahariri wa habari kuvipa kipaumbele vipindi na
habari zinazohusu Kipindupindu katika vyombo vyao ili wananchi waweze
kuzinduka.
Nae Ofisa Afya kutoka Shirika la
Afya Duniani (WHO) Ofisi ya Dar es salaam Dkt. Neema Kileo ameshauri
vipindi vinavyozungumzia kipindupindu vipangwe katika muda ambao
wananchi wengi wanaweza kuvisikiliza.
Washiriki wa mafunzo hayo
wamekubali kutoa muda zaidi katika vyombo vyao vya habari kwa maafisa
wa Kinga na Elimu ya Afya ili kutoa elimu zaidi katika kukabiliana na
maradhi hayo.
0 maoni:
Chapisha Maoni