Spika wa Bunge, Job Nduga |
FALSAFA
ya Rais John Magufuli ya Hapa Kazi Tu imeanza kutekelezwa bungeni baada
ya jana, Bunge kutengua baadhi ya kanuni zake ili wawe na muda mwingi
zaidi wa kufanya kazi; kitendo ambacho Spika wa Bunge ameomba Watanzania
wote kufuata nyayo za mhimili huo.
Aidha,
Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano umepitishwa na Bunge, huku
wabunge wakieleza kuwa na imani kubwa ya kutekelezwa kwa kile
kilichoelezwa ni nidhamu iliyojengwa kwa muda mfupi na Rais Magufuli
katika utumishi wa umma.
Uamuzi wa
kuongeza muda wa majadiliano kutoka saa 10 hadi saa 2 usiku,
ulipitishwa jana na wabunge baada ya hoja husika kuwasilishwa na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na
Walemavu, Jenista Mhagama.
Waziri
Mhagama aliwasilisha pia pendekezo la serikali la kutengua kanuni Bunge
liendelee na vikao vyake Jumamosi badala ya kusitisha Ijumaa.
Pia
alipendekeza Mawaziri kupewa dakika 45 kusoma hotuba zao za bajeti na
dakika 50 wakati wa kuhitimisha hotuba hizo. Kanuni za Bunge zinalitaka
Bunge kuanza vikao vyake saa 3:00 asubuhi hadi saa 7:00 mchana ambapo
husitishwa na kurejea saa 11:00 jioni mpaka saa 2:15 usiku.
Pia kanuni za Bunge zinalitaka Bunge kusitishwa Ijumaa hadi Jumatatu.
Akijenga
hoja hiyo iliyopitishwa kwa kishindo na Bunge, Waziri Mhagama alisema
lengo ni kuwezesha Bunge kufanya kazi kubwa zaidi na kukamilisha kazi
zote za Bajeti itakayosomwa Juni 9 mwaka huu katika muda muafaka sawa na
mabunge mengine ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Kwa
kuzingatia kwamba vikao vya Mkutano huu wa Bunge vilianza Aprili 19
mwaka huu na kwa vile vitaendelea hadi Julai Mosi, mwaka huu, Bunge
linalazimika kutengua baadhi ya kanuni zake ikiwepo kanuni ya 105, ili
kuweza kumaliza kazi zake katika muda uliopangwa,” alisema Waziri
Mhagama.
Akizungumza
mara baada ya Bunge kutengua kanuni hizo, Spika wa Bunge, Job Ndugai
alisema mabadiliko hayo yanalenga kuliwezesha Bunge kuendana na falsafa
ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ‘Hapa Kazi Tu’.
“Nawashukuru
sana wabunge kwa kukubali kwa kauli moja kutenguliwa kwa kanuni hizi za
Bunge ili kutupa muda mwingi zaidi wa kuchapa kazi na nawaomba
Watanzania wote waige mfano huu wa Bunge wa kumuunga mkono Rais katika
suala la uchapaji kazi,” alisema Ndugai.
Imani kwa JPM
Kabla ya
kupitishwa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wabunge wengi
walisema wana imani kubwa ya utekelezaji wa mpango huo.
Mambo
yaliyowaaminisha wabunge wengi yaliegemea katika nidhamu ya matumizi ya
umma, ulipaji wa kodi, mawaziri kuiga utendaji wa Rais, ufuatiliaji
katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo maji, kilimo, afya, elimu,
miundombinu na uwajibikaji uliohuishwa serikalini.
Wakati
Mpango wa miaka mitano unaomalizika wenye thamani ya Sh trilioni 44.5
umetajwa kutekelezwa na serikali kwa kiwango cha asilimia 60 , wabunge
wengi wamesema wana imani na Mpango huo wa awamu ya kwanza ya utawala wa
Rais Magufuli wenye thamani ya Sh trilioni 107, utatekelezwa kwa
ufanisi mkubwa.
Wakijadili
mpango huo uliowasilishwa juzi na kuhitimishwa jana na Waziri wa Fedha
na Mipango, Dk Philip Mpango, wabunge walisema kwa namna Dk Mipango
alivyoainisha vipaumbele vya maendeleo ni wazi kwamba sasa dira ya
kulifikisha taifa katika uchumi wa kati inaonekana dhahiri.
Mbunge wa
Kisesa, Dk Raphael Chegeni (CCM) alisema nidhamu ya uwajibikaji
serikali, ikiwa ni pamoja na kasi ya utumbuaji wa majipu ambayo
imewafanya Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuwajibika na kuogopa
kujihusisha na rushwa na ufisadi hatua itakayolipaisha Taifa.
“Mheshimiwa
Spika, sekta ya umma ni tatizo kubwa katika nchi hii na dawa pekee ni
utumbuaji wa majipu, ni lazima Watanzania wote tumuunge mkono kwa nguvu
zetu zote Rais Magufuli katika utumbuaji wa majipu, kila mahali
yalipoota ni lazima yatumbuliwe nchi iende,” alisema Dk Chegeni.
Akizungumzia
nidhamu katika ulipaji wa kodi, Mbunge huyo alisema ndani ya muda mfupi
nidhamu katika kulipa kodi imeanza kurejea tofauti na zamani ambapo
wafanyakazi ndio waliokuwa wakilipa kodi huku wafanyabiashara wakiona
suala la kulipa kodi ni sawa na uzembe.
Alisema
mfano wa wazi kabisa unaodhihirisha utekelezaji wa Mpango huo ni hatua
ya kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kutoka Sh bilioni 850 hadi Sh
trilioni 1.3 kwa mwezi katika uongozi wa Rais Magufuli, lakini akasema
ni lazima mianya zaidi katika ukwepaji wa kodi idhibitiwe huku akizitaja
kampuni za simu kuhusika kwa kiasi kikubwa na ukwepaji wa ulipaji wa
kodi halali za serikali.
“Mheshimiwa
Spika hili la kampuni za simu ni lazima tulitafutie dawa. Nakumbuka
TCRA (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania), iliwahi kuwaeleza TRA (Mamlaka
ya Mapato Tanzania) namna ya kukusanya kodi kwa kampuni za simu. Ni
lazima mfumo uliopo ubadilishwe haraka ili kuzuia ukwepaji kodi.
“Ukiondoa ukwepaji kodi katika biashara zao lakini pia kuna hili suala
la minara ya simu. Minara hii imejengwa kila mahali vijijini, lakini
halmashauri za wilaya hazinufaiki na uwepo wa minara hii, wakati umefika
sasa wa kulitazama upya hili,” alisema Chegeni.
Mbunge wa
Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM), Mbunge wa Mbogwe Agustino
Masele (CCM), Mbunge wa Busanda, Lolensia Bukwimba (CCM), Mbunge wa
Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema) walijielekeza zaidi katika
kuishauri serikali kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo maji, elimu,
afya, miundombinu na kilimo.
Kanyasu
alisema kinachompa matumaini ya Mpango huo kupata mafanikio makubwa ni
hatua ya Mawaziri kuanza kuiga mtindo wa uchapaji kazi wa Rais Magufuli
akisema hatua hiyo itaharakisha sana katika kutatua matatizo mengi ya
wananchi masikini, lakini pia akaeleza kuridhishwa na nidhamu katika
ulipaji wa kodi hivi sasa.
Mbunge wa
Mkuranga, Abdalah Ulega (CCM) alisema ili mpango huo uweze kufanikiwa
na kuifanya nchi kuelekea katika uchumi wa viwanda utakaoivusha kirahisi
kuelekea uchumi wa kati, suala la kutengwa maeneo maalumu ya viwanda
halikwepeki, akisema hatua hiyo pamoja na mambo mengine itahuisha
ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Mbunge wa
Malindi, Ally Saleh (CUF) aliitaka serikali kuelekeza macho yake katika
kuendeleza Ukanda wa Mtwara akisema ukanda huo una utajiri usiopimika
na ambao unaweza kuiondoa nchi katika umasikini uliopo.
Alipendekeza
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi
ili kubaini ukweli wa kiwango cha deni la Taifa kutokana na kuwepo kwa
taarifa zinazokinzana na kuongeza kwamba mataifa mengi yameporomoka
kutokana na kushindwa kujua madeni yao ya taifa na namna ya kuyapatia
ufumbuzi.
Alisema
pamoja na kwamba Mpango unaelezea kukuza pato la Mtanzania kutoka Dola
1006 kwa mwaka kwenda 1,500, mkakati huo hautaweza kufanikiwa kwa
kutupia macho sekta ya viwanda peke yake na badala yake maeneo ya
kilimo, uvuvi, rasilimali za Mtwara kama gesi na pia ufufuaji wa Shirika
la Ndege (ATCL) yatiliwe mkazo.
0 maoni:
Chapisha Maoni