Wanadamu
wameumbwa kwa hulka na silika ya kuwa na uwezo wa kuwasiliana miongoni
mwao, jamii wanamoishi, taifa na hata ulimwenguni ili waweze kutimiza
nia na azma yao ya kuwasiliana.
Ili mawasiliano hayo yakamilike ni lazima yabebe ujumbe unaokusudiwa kufikishwa katika jamii.
Ujumbe
huo ili uweze kumfikia mlengwa, ni lazima iwepo njia ya kuufikisha
ujumbe huo kwa mlengwa ambao huwasilishwa kwa maandishi (magazeti),
sauti (redio) na picha (TV) pamoja na mitandao ya kijamii kupitia huduma
ya inteneti.
Vyombo
hivyo vya habari vinahusisha wataalamu ambao kazi yao ni kuhakikisha
jamii inapata ujumbe kwa wakati ili kuweza kujenga, kuboresha na
kuimarisha maisha yao kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.
Vyombo
vya habari hakika vimekuwa ndio macho na masikio ya wananchi ili
kufikisha ujumbe unaohusu mambo mbalimbali yanayofanyika ndani na nje ya
nchi.
Tunapoelekea
siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo
huadhimishwa kila mwaka Mei 2 na 3, maadhimisho hayo mwaka huu
yataadhimishwa nchini Finland, ambapo wanahabari wote duniani wataungana
kuwakumbuka wenzao waliofariki dunia walipokuwa wakitekeleza majukumu
yao na kupanga mipango mipya ya namna watakavyoboresha kazi zao ziwe za
ufanisi zaidi.
Tanzania ikiwa miongoni mwa mataifa ya dunia hii, nayo haipo nyuma katika suala la uwepo wa vyombo vya habari.
Ni
dhahiri vyombo vya habari nchini vimekuwa kiungo muhimu katika kisaidia
Serikali kutoa taarifa mbalimbali na ajira hatua ambayo imesaidia
kupunguza tatizo la ajira nchini.
Ukilinganisha
na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania inayoongoza kwa kuwa na
vyombo vingi vya habari, hali ambayo ni msingi wa kuajiri watu wengi
zaidi katika tasnia hiyo.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye ambaye ndiye mwenye
dhamana ya habari nchini anasema Serikali inaunga mkono juhudi
zinazofanywa na vyombo vya habari nchini.
“Tulipofika
ni pazuri ukilinganisha na tulipotoka, mengi yamefanyika hasa
ukiangalia idadi ya vyombo vya habari nchini na uhuru wa waandishi wa
habari wanavyoanadika na wanavyofikisha ujumbe kwa wasomaji,
wasikilizaji na watazamaji” alisema Waziri Nape.
Aidha,
Waziri Nape amesema kuwa bado Serikali inakusudia kuboresha mazingira
ya waandishi wa habari ili waweze kufanya kazi zao kwa hali ya uhuru
hasa wanapotimiza majukumu yao ya kiundishi wa habari.
Kwa
mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambacho ni
chombo kilichoanzishwa kisheria kusimamia sekta za mawasiliano na
utangazaji nchini hadi sasa kuna jumla ya vituo kadhaa vya radio na
televisheni vilivyosajiliwa.
Idadi
ya vituo vya redio vilivyosajiliwa nchini hadi sasa ni 123 ambavyo ni
sawa na asilimia 43.4 katika ukanda wa Afrika Mashariki huku miongoni
mwa vituo hivyo vinamilikiwa na makampuni binafsi, taasisi na mashirirka
ya dini, jamii na Serikali ambayo inayomiliki kituo kimoja cha TBC
Taifa inayoendeshwa chini ya Shirika la Taifa la Utangazaji (TBC),
nchini Kenya vipo vituo vya redio 118 sawa na asilimia 41.7, Uganda 37
sawa na asilimia 13.1, Rwanda vituo vitatu sawa na asilimia 1.1 wakati
Burundi ina vituo vya redio viwili ambavyo ni sawa na asilimia 0.7.
Kwa
upande wa vituo vya televisheni, Uganda inaongoza kwa kuwa na vituo
vingi ambavyo idadi yake ni 44 sawa na asilimia 53.6, ikifuatiwa na
Tanzania yenye vituo 24 sawa na asilimia 29.3, Kenya vituo 10 sawa na
asilimia 12.2, Rwanda vituo vitatu ambavyo ni sawa na asilimia 3.7 na
Burundi ikiwa na kituo kimoja cha televisheni ambacho ni sawa na
asilimia 1.2
Kwa
kuzingatia maslahi ya wananchi na wamiliki wa vyombo vya habari na
wanahabari wenyewe, TCRA imekuwa ikihimiza juu ya ufanisi wa ushindani
na uchumi, kulinda maslahi ya walaji, kulinda uwezo wa fedha na ufanisi
wa wagavi.
Pia
inahimiza upatikanaji wa huduma zinazosimamiwa kisheria kwa walaji
wakiwemo wenye kipato cha chini na walaji wa vijijini na wa pembezoni,
kukuza mwamko, maarifa na uelewa wa jamii kuhusu sekta zinazosimamiwa
ikiwemo kuzingatia haja ya kulinda na kuhifadhi mazingira, haki na
wajibu wa walaji na wagavi wanaosimamiwa.
Katika
kuonesha Tanzania inavyosimamia uhuru wa vyombo vya habari, TCRA ina
jukumu lingine la kusimamia malalamiko na migogoro inayoweza kujitokeza
miongoni mwa wateja wake wakiwemo wamiliki wa vyombo vya habari,
wananchi na kupatia ufumbuzi changamoto hizo.
Aidha,
hadi Aprili 22, 2016, Tanzania imekuwa ndio nchi inayoongoza Afrika
Mashariki kwa kuwa na idadi kubwa ya magazeti yaliyosajiliwa ambapo
idadi yake ni 881 licha ya magazeti na majarida mengi kusajiliwa, mengi
huchapishwa mara chache na mengine kutokuchapishwa na kusambazwa baada
ya kusajiliwa.
Kwa
idadi ya magazeti nchi za Uganda, Rwanda na Burundi yapo magazeti
matano yanayotumika katika nchi hizo wakati Kenya ina magazeti saba
ambayo husomwa na kufikisha ujumbe kwa walengwa katika mataifa hayo.
Wingi
huo wa vyombo vya habari nchini imekuwa ishara njema ya kujali uhuru wa
kuanzishwa kwa vyombo vya habari kwa makampuni binafsi, taasisi na
mashirika ya dini pamoja na jamii mbalimbali ili kuweza kuwa ndio namna
yao ya kupata taarifa.
Katika
ulimwengu wa leo, uhuru wa habari ni suala la msingi na lina umuhimu
mkubwa katika kutekeleza haki za binadamu katika kutafuta, kupata,
kupokea na kutoa habari ambazo ni muhimu kwa nchi katika kujiletea
maendeleo endelevu.
Kauli
mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inawahimiza wanahabari na watu wote
kutambua “Kupata Habari ni Uhuru wa Kimsingi: Hii ni haki yako!”
ikilinganishwa na kauli mbiu ya mwaka uliyopita ambayo ilisema “Achia
uwandishi habari ustawi! Kuelekea upashaji habari bora, usawa wa jinsia
na usalama wa vyombo vya habari katika enzi ya dijitali”.
Kwa
mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Shirika la
Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) Aprili 8, 2016
imebainisha kuwa katika maadhimisho ya Siku ya vyombo vya habari duniani
mwaka huu, mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka Azerbaijan Khadija
Ismayilova amechaguliwa kupokea tuzo ya uandishi wa habari za uchunguzi
ijulikanayo “Guillermo Cano” inayotolewa na Shirika hilo.
Tuzo
hiyo ina thamani ya Dola za Kimarekani 25,000, na imepoewa jina hilo
kwa heshima ya Guillermo Cano Isaza, mwandishi wa habari wa Colombia
aliyefariki Desemba 17, 1986 akiwa kazini.
Jukumu
la kuenzi na kutoa tuzo ya heshima kwa waandishi wa habari duniani
linafadhiliwa na taasisi ya Cano Foundation kutoka nchini Colombia na
Helsingin Sanomat Foundation kutoka nchini Finland.
Msaidizi
wa Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Habari UNESCO Frank La Rue anasema
“Uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwa taarifa muhimu na uwazi ni
ambao ni mahitaji ya jamii ya kidemokrasia. Lakini leo tunaona ongezeko
la ghasia na vitisho dhidi ya waandishi ambayo mimi napendekeza nchi
zote duniani kuanzisha utaratibu wa habari na ulinzi kwa ajili ya
usalama wa waandishi wa habari”
Moja
ya changamoto za kuweka utaratibu wa usalama wa waandishi wa habari ni
idadi ndogo ya mifano ya taratibu zilizopo ambayo inaweza kuwa somo ili
wengine waweze kujifunza kutokana na taratibu zilizopo.
Masuala
muhimu ya kuzingatiwa wakati wa kuanzisha utaratibu huo ni pamoja na
kuwepo kwa makundi matatu ambayo ni wigo wa utaratibu, ushirikishwaji wa
wadau muhimu pamoja na taasisi kubuni na kutathmini hatua ambayo
itasaidia kufikia malengo ya kumlinda mwandishi wa habari.
Akizungumzia
maandalizi ya maadhimisho kitaifa ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya habari
nchini ambayo yanafanikia jijini Mwanza Mei 2 na 3, mwaka huu,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo Andrew Marawiti
amesema kuwa yanaendelea vizuri kulingana na ratiba ilivyopangwa.
Katika
maadhimisho hayo, Marawiti amesema kuwa Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Othman Chande ambapo wakati
wa ufunguzi wa maadhimisho hayo mada mbalimbali zitawasilishwa na
watoaKuhusu ratiba ya siku mbili za maadhimisho hayo, Marawiti amesema
kuwa zitawasilishwa zikiandamana na majadiliano kwa washiriki wote.
Miongoni
mwa washiriki wanaotarajiwa kuwepo katika maadhimisho hayo ni wadau
mbalimbali wa habari wakiwemo viongozi wa Serikali, Mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wawakilishi wa Mashirika ya
Kimataifa, wamiliki wa vyombo vya habari, waandishi wa habari na
wananchi.
Kulingana
na takwimu zilizopo, mwandishi wa habari mkongwe nchini, Mzee Willie
Mbunga amesema kuwa Tanzania ina vyombo vingi vya habari ikilinganishwa
na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo kulikuwa vyombo vichache vya
habari ambavyo ni redio Tanzania Dar es salaam, Tanganyika Standard,
Mambo Leo, Uhuru, Mzalendo na Ngurumo.
Aidha,
amesema kuwa changamoto ya baadhi ya watu kujisahau na kuweka pembeni
maadili ya uandishi wa habari ni suala ambalo si la kufumbiwa macho, ni
vema litiliwe maanani ili kukiokoa kizazi cha sasa na kijacho katika
kujenga jamii inayojali na kusimamia maadili ya taaluma na ya jamii.
Katika
upashanaji habari, dunia sasa imekuwa sawa na kijiji hasa katika
kipindi hiki cha sayansi na teknolojia ambapo mawasiliano ndio imekuwa
nguzo ya kila kitu.
Awali
makala haya yameonesha kuwa ujumbe katika jamiiulifikishwa kwa njia ya
redio, magazeti na TV, zaidi ya vyombo hivyo, mitandao ya kijamii kwa
sasa imekuwa nguzo mahiri na vyanzo vikuu vya habari kwa waandishi wa
habari na wananchi.
Miongoni
mwa mitandao hiyo ya kijamii ni pamoja na blog ya Serikali, Michuzi,
fullshangwe, bayana, milardayo, mwamba wa habari, businessmagnetblogs,
mpekuzi, moh Dewji na mitandao mingine.
Mwandishi
wa habari Majid Mjengwa ambaye pia ni mwanzilishi na mmiliki wa blog ya
mjengwa anasema “Mitandao ya kijamii imekuwa ni eneo la upashanaji
habari linalofanya kazi kama vyombo vingine vya habari”.
Ili
kufikisha ujumbe kwa jamii, Mjengwa amesema kuwa watu wote wanaofanya
kazi katika mitandao ya kijamii wanapaswa kufuata maadili ya taaluma ya
habari pamoja na sheria na taratibu za nchi husika ili kuondoa mgongano
wa maslahi katika kufikisha ujumbe kwa jamii.
Ni
dhahiri haki na wajibu ni vitu ambavyo haviachani, hivyo ni jukumu la
kila mdau wa habari nchini wakiwemo Serikali, waandishi wa habari,
wamiliki wa vyombo vya habari na wananchi kuzingatia sheria, kanuni,
taratibu pamoja na maadili ya jamii.
Hatua
hiyo itasaidia kuimarisha na kuhakikisha wadau hao wanakuwa sehemu ya
kujenga uhuru wa vyombo vya habari ambavyo vitakuwa chachu ya kujenga
taifa imara lenye uchumi bora kwa manufaa ya Watanzania ifikapo mwaka
2025.
Imeandaliwa na Eleuteri Mangi-MAELEZO
0 maoni:
Chapisha Maoni