Shirika lisilo la kiserikali la Sustainable Environment Management Action (Mpango endelevu wa uboreshaji mazingira – SEMA) la mkoani hapa, limetumia zaidi ya shilingi 562.4 Milioni kugharamia mradi wa Mwanzo Mwema kati ya Aprili mwaka jana hadi sasa.
Mradi huo utatekelezwa katika wilaya ya Iramba (kata 11) na Manispaa (10), unafadhiliwa kwa pamoja na WaterAid Tanzania, Amref Health Africa, RFSU na SEMA ni mtekelezaji mkuu.
Hayo yamesemwa juzi na Meneja Mkuu wa SEMA, Ivo Manyaku, wakati akitoa taarifa yake kwenye warsha iliyohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya huduma za jamii mkoani hapa, iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa manispaa ya Singida.
Alisema kati ya fedha hizo, shilingi 423,020,365 zimetumika wilayani Iramba ambazo zimegharamia ukarabati wa majengo, uboreshaji wa miundombinu ya maji na usafi wa mazingira katika hospitali ya wilaya ya Iramba iliyoanzishwa 1967. Pia, vituo vya afya vya Ndago na Mgongo vimefanyiwa ukarabati.
“Kwa Manispaa tumetumia shilingi 139,401,221 ambaz,o tumezitumia kuboresha miundombinu, ukarabati wa majengo na ununuzi wa vifaa vya usafi wa mazingira, katika hospitali za mkoa, kituo cha afya cha Sokoine na Zahanati ya Mwankoko,” alisema Manyaku.
Kuhusu mradi wa ‘Mwanzo Mwema’, alisema mradi huo ulioanza Aprili mwaka jana na unatarajiwa kufikia kikomo chake Machi mwaka (2017), unalenga kuboresha huduma za afya ya uzazi na ujinsia katika jamii.
“Aidha, mradi huu ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupunguza vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi. Aidha malengo mahususi ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi katika vituo vya kutolea huduma za afya na katika Shule,” alisema Manyaku.
Kwa upande wake ofisa tathmini na ufuatiliaji TMEP ID,George Mutasingwa, alisema lengo mahususi la mradi wa Mwanzo Mwema ni uhamasishaji wa ushirika wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na kupinga ukatili wa kijinsia.
Naye meneja mawasiliano wa shirika la RFSU TMEP, Euginia Msasanuri pamoja na mambo mengine, alisema ni wajibu kwa wanaume kuona umuhimu wa kuwasindikiza wenza wao kliniki ili waweze kushirikishwa endapo ujauzito wa mweza ukiwa na matatizo.
Aidha, Meneja Msasanuri, ametumia fursa hiyo kuitaka jamii kujenga utamaduni wa kuipokea na kuiendeleza miradi inayotekelezwa na wafadhili kwenye maeneo yao ili iweze kunufaisha jamii kwa muda mrefu zaidi.
Na Nathaniel Limu, Singida
IMG_4767
Afisa tathmini na ufuatiliaji TMEP ID, George Mutasingwa akitoa taarifa yake mwenye warsha ya wajumbe wa kamati ya huduma za jamii Manispaa ya Singida juzi. Pamoja na mambo mengeine, Mutasigwa alidai kwamba upo umuhimu mkubwa kwa wanaume kushiriki masuala ya afya ya uzazi. Warsha hiyo ilifanyikia kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya manispaa ya Singida.
IMG_4770
Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la SEMA mkoani Singida,Ivo Manyanku, akitoa nasaha zake kwenye warsha ya wajumbe wa kamati ya huduma za jamii mkoa wa Singida.
IMG_4773
Baadhi ya wanakikundi cha ushawishi na utetezi mkoa wa Singida waliohudhuria mkutano wa kubadilishana uzoefu kuhusu afya ya uzazi na usafi wa mazingira.
IMG_4778
Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii Manispaa ya Singida na diwani wa kata ya Mungumaji, Hassan Mkata, akifungua mkutano wa ushawishi na utetezi wa masuala ya afya ya uzazi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Ruruma mjini Singida  (Picha na Nathaniel Limu)
IMG_4794
Meneja wawasiliano shirika la RFSU TMEP, Euginia Msasanuri, akizungumza na kikundi cha ushawishi na utetezi wa masuala ya afya ya uzazi na ujinsia waliohuduhuria mkutano wa kuhamasisha afya ya uzazi.
IMG_4796