Jumatano, 27 Aprili 2016

MJANE WA MWALIMU BABA WA TAIFA MAMA MARIA ATEMBELEA DARAJA LA NYERERE KIGAMBONI LEO


 

mama1Mama Maria Nyerere, Mjane wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,  akiwa na mwanae Mhe. Makongoro Nyerere na msaidizi wake akifurahia mandhari wakati walipotembelea Daraja la Nyerere Kigamboni jijini Dar es salaam. Mama Maria, ambae hakujali mvua kubwa iliyokuwa inanyesha, alionekana mwenye furaha kufika darajani hapo kwani ndoto ya miaka  mingi iliyoanzishwa na hayati mumewe imetimia. Pia alimshukuru sana Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kuagiza daraja lipewe jina  la Mwalimu na siyo yeye, jambo ambalo amesema limemfariji sana kwani vizazi vya sasa na nvijavyo vitamkumbuka mwasisi wa Taifa..
PICHA NA IKULU
mama2 mama3Mke wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Maria Nyerere ametembelea Daraja la Nyerere linalounganisha eneo la Kigambaoni na Kurasini Jijini Dar es salaam na kuipongeza serikali na wananchi wote wa Tanzania kwa kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo kubwa na la kisasa kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.
Mama Maria Nyerere aliyeongozana na Mwanae Mheshimiwa Makongoro Nyerere amesema kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 254.12 kumekamilisha mpango wa miaka mingi ulioanzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa na nia ya kujenga daraja katika eneo hilo la mkondo wa bahari lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti haikuwezekana.
Aidha, Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere  kwa heshimu ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na amebainisha kuwa uamuzi huo utaviwezesha vizazi vijavyo kutambua juhudi zilizofanywa na mmewe katika ujenzi wa nchi.
“Mimi ninamshukuru sana Rais kwa maana ilikuwa lipewe jina lake, lakini yeye Mungu akamjaalia akasema kwamba hapana tukumbuke tulikotoka, kwa hiyo najisikia vizuri sana, na familia nayo inajisikia vizuri sana, lakini zaidi na watanzania wanajisikia vizuri sana, kwa maana watakuwa wanaulizana Nyerere alikuwa ni nani?” Amesisitiza Mama Maria Nyerere.
Daraja la Nyerere lenye urefu wa meta 680, upana wa meta 32, njia sita za magari na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5, lilifunguliwa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Aprili, 2016 na linakuwa kiunganishi muhimu kati ya Kigamboni na katikati ya Jiji la Dar es salaam.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
27 Aprili, 2016
.

0 maoni:

Chapisha Maoni