Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Kampuni ya Moovn Tanzania Limited imeboresha
huduma za usafiri na kuongeza usalama wa wateja kwa kuanzisha huduma za
usafiri zinazopatikana kwa njia ya mtandao.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo,Bw.Godwin Ndugulile alipokua
akiwaelekeza waandishi wa habari jinsi ya kujiunga na huduma za usafiri
kwa njia ya mtandao.
“Huduma zetu za usafiri zinapatikana kwa
njia ya simu na tovuti kupitia program za aina tatu ambazo ni programu
inayomuhusu mteja,(Moovn Passenger), programu inayomuhusu dereva (Moovn
Driver) pamoja na Programu inayohusiana na mashirika au makampuni ya
kibiashara”alisema Bw.Ndugulile.
Bw.Ndugulile ameongeza kuwa huduma hizo
zinapatikana bure kwa wateja wote pia kampuni inashirikiana na madereva
wa vyombo vya usafiri wa aina zote zikiwemo taxi, pikipiki, na bajaji
ili kutoa huduma nafuu kwa wateja wao.
Aidha, Bw. Ndugulile amezitaja baadhi ya
faida zinazopatikana kwa kutumia huduma hii kuwa ni; usafiri wa uhakika
kwa kuwa madereva wote wana leseni na wamesajiliwa, usalama, bei nafuu
kulingana na mahitaji na uwezo wa mteja, pamoja na kuongeza ajira na
kipato kwa madereva.
Kampuni ya Moovn Tanzania Limited
imeanza kufanya kazi rasmi Machi 16 Mwaka huu, Ofisi zake zinapatikana
maeneo ya Osterbay Jijini Dar es Salaam pia Kampuni ina mpango wa
kufungua matawi mengine nchi nzima.
0 maoni:
Chapisha Maoni