Rais John Magufuli ametoa msamaha kwa wafungwa 3,551, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Muungano wa Tanzania iliyoadhimishwa tarehe26 /4/2014 .
Taarifa
hiyo iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja
Jenerali Projest Rwegasira ikisema wafungwa 580 wataachiwa huru, huku
wengine 2,971 watapunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao.
Alisema
rais ametoa msamaha huo kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya ibara
ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aliwataja
watakaonufaika na msamaha huo kuwa ni wafungwa wenye ugonjwa wa ukimwi,
kifua kikuu na saratani ambao wapo kwenye hatua za mwisho. Wengine ni
wazee wenye umri wa miaka 70 na kuendelea, wajawazito na wale waliongia
na watoto gerezani.
Wafungwa wengine watakaonufaika na msamaha
huo ni wenye ulemavu wa akili ambao wamethibishwa na jopo la waganga
kuwa wana tatizo hilo.
Katibu mkuu wa wizara hiyo alisema
msamaha huo hautawagusa wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa au
kifungo cha maisha jela.
Pia, wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, upokeaji na
utoaji rushwa, matumizi mabaya ya madaraka, unyang’anyi kwa kutumia
silaha na kubaka ni miongoni mwa waliokosa msamaha huo.
Wengine
ambao hawataguswa na msamaha huo ni wale wanaotumikia vifungo kwa makosa
ya kupatikana na silaha, wizi wa magari na pikipiki, kuwapa mimba
wanafunzi na ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Wafungwa wengine
watakaoendelea kubaki magerezani ni wale waliohukumiwa kutokana na
usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili, utekaji wa watoto,
biashara ya binadamu, kukutwa na viungo vya binadamu na waliojaribu
kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.
Katika maadhimisho ya Uhuru
yaliyofanyika Desemba 9, 2015, Rais Magufuli aliwasamehe wafungwa 2,336,
kati ya hao 117 waliachiwa huru huku 2,219 wakipunguziwa moja ya sita
ya vifungo vyao.
Kwa idadi hiyo mpaka sasa wafungwa 5,887
wamenufaika na msamaha wa Rais Magufuli tangu aingie madarakani baada ya
kushinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2015.
0 maoni:
Chapisha Maoni