ASILIMIA 70 ya mazao ya misitu hupotea
wakati wa uvunaji kwasababu ya matumizi ya teknolojia iliyopitwa na ujuzi mdogo
kwa baadhi ya watendaji wa sekta hiyo jambo linalopunguza mapato kwa wadau wa
sekta hiyo na serikali.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo,
Programu ya Panda Miti Kibiashara (PFP) kwa kushirikiana na Wataalamu wa
Mitaala (curricula experts) wameandaa mitaala ya misitu na viwanda vya misitu
itakayotumiwa na wadau katika ngazi ya vyuo vya ufundi stadi ili kupata
watendaji watakaongeza tija katika sekta hiyo.
Akizungumza katika mkutano uliojadili
mitaala hiyo hivikaribuni mjini Iringa, Afisa Mafunzo wa Programu ya Panda Miti,
Julius Sonoka alisema wadau wa sekta hiyo wataendelea kupata hasara kubwa kama
wataendelea kutumia mashine za kizamani katika uvunaji.
Alisema utafiti unaonesha matumizi ya
mashine za kisasa yanasaidia kupunguza upotevu wa mazao ya misitu kutoka asilimia 70 hadi 30 jambo linaloifanya
sekta hiyo iwe na tija zaidi.
Sonoka alisema kukamilika kwa mitaala
hiyo kutawawezesha wavunaji na wafanyakazi wengine wa sekta hiyo kupata
ujuzi utakaoboresha kazi zao tofauti na ilivyosasa ambapo wengi wao
wanafanyakazi kwa kutumia uzoefu.
“Mitaala hii itawawezesha wadau kuongeza
ujuzi katika kuihudumia sekta hii kwa kupitia mfumo rasmi ya elimu unaotolewa
katika vyuo vya ufundi stadi,” alisema.
Katibu wa Chama cha Wavunaji wenye Viwanda
vya Mbao katika Msitu wa Saohill Mufindi (SAFIA), William Mgowole alisema wavunaji
wengi wanatumia mashine aina ya digdong na kuingia katika hasara inayozungumzwa
kwasababu nyingi ya mashine hizo teknolojia yake ni ya kizamani.
Mgowole alisema ili kupeukana na hasara
hiyo wavunaji wanashauri kutumia mashine za kisasa aina ya bed saw zinazosaidia
kudhibiti upotevu wa mazao ya misitu chini ya asilimia 30.
Rais wa
Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania (Shivimita), Ben Sulusi alisema kuna
jumla ya viwanda 300 vya mazao ya misitu nchini na kati yake 70 ni vikubwa ambavyo
vinatumia mashine za kisasa na vilivyobaki 230 vinatumia mashine za zamani zinazoruhu
upotevu mkubwa.
Akizungumzia umuhimu wa mitaala hiyo
alisema itasaidia uzalishaji wa malighafi bora kwani itatoa wataalamu wa miti
kuanzia upandaji, uvunaji mpaka kiwandani na kuwa itaondoa matumizi ya
wafanyakazi wasiokuwa na ujuzi wowote kwenye sekta hiyo.
Naye Afisa Misitu Mkuu wa Msitu wa Taifa
(Sao Hill), Salehe Bereko alisema wadau wa misitu wataweza kupata taaluma
sahihi na kuongeza uzalishaji na kutosheleza mahitaji ya soko la ndani na nje.
Alisema kutokana na kupungua kwa mgao wa
uchakataji wa mazao ya misitu kutoka meta za ujazo milioni moja mpaka 600,000
kwa mwaka upandani wa miti kitaalamu na matumizi ya teknolojia ya kisasa
inayopunguza upotevu wa mazao wakati wa uchakataji ndio njia sahihi ya kukabiliana
na changamoto hiyo.
Naye Mhandisi Julius Mwakasasa kutoka
Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) ambaye ni mkufunzi wa mitambo alisema VETA ipo
tayari kushirikiana na wadau kuzalisha watendaji wa sekta hiyo wenye ujuzi
watakaofanya kazi zao kwa weledi na viwango chini ya wasimamizi wenye taaluma
ya kutosha ya misitu.






0 maoni:
Chapisha Maoni