Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Biashara na Viwanda wa
Singapore, Dkt. Koh Poh Koon (kulia kwake) na ujumbe wake, Ofisini
kwake bungeni mjini Dodoma Aprili 27, 2016. Kulia ni Waziri wa Viwanda
na Biashara, Charles Mwijage.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Biashara na Viwanda wa
Singapore, Dkt. Koh Poh Koon (kulia ) na ujumbe wake kabla ya
mazungumzo yao , Ofisini kwake bungeni mjini Dodoma Aprili 27, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………………………….
WAZIRI wa Biashara na Viwanda wa
Singapore, Dk. Koh Poh Koon, amesema wamepanga kutumia bandari ya Dar es
Salaam kuwa kiunganishi cha biashara kati ya nchi hiyo na mataifa
mengine ya Afrika Mashariki.
Dk. Koon ameyasema hayo leo
(Jumatano, Aprili 27, 2016), wakati alipomtembelea Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma, na kwamba Singapore ipo tayari
kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari
ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za
Tanzania.
Dk. Koon ambaye ameambatana na
wafanyabiashara wakubwa wapatao 40, amemweleza Waziri Mkuu kwamba
kampuni ya Hyflux ya Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo
maalum la uchumi (Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya
kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya
kuweka viwanda vya kati (light industries), maeneo ya biashara na nyumba
za makazi zipatazo 37,000.
“Jiwe la msingi la mradi huo
litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na
Uwekezaji, Charles Mwijage,” alisema.
Mbali na ushirikiano katika sekta
ya biashara na uwekezaji, Dk Koon amweleza Waziri Mkuu kwamba nchi yake
itaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali
ya menejimenti na uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi
na mafuta.
“Hadi sasa makampuni ya Singapore
yaliyowekeza nchini ni pamoja na Pavillion Energy ambayo imewekeza
kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 1.2 katika sekta ya gesi na
inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani bilioni 3 kwa ajili ya
ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant) kitakachojengwa mikoa ya
Kusini kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na Marekani”.
Amesema kampuni ya PIL ya
Singapore inatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 400 kwa ajili
ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa makampuni ya gesi.
Amesema lengo la ziara hiyo ni
kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo pamoja na kuweka mikakati
ya kuinua uchumi na kupanua wigo wa biashara.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu
Majaliwa ameishukuru Serikali ya Singapore kwa uwekezaji unaofanywa na
makampuni yake nchini na kwa misaada ya kiufundi ambayo wameitoa kwa
Tanzania katika nyanja mbalimbali.
Ili kusaidia juhudi za Serikali
ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Waziri Mkuu ameyakaribisha makampuni
mengine ya Singapore kuja nchini kufanya uwekezaji katika maeneo
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda, mahoteli, kilimo na
nishati.
Amemuahidi Dk. Koon kwamba
Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia
na kulinda uwekezaji baina ya nchi mbili (Bilateral Investment
Protection and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru
mara mbili (Double Taxation Avoidance Agreement) ili kuvutia uwekezaji
zaidi kutoka Singapore.
Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka
Watanzania kutumia fursa ya ushirikiano kati ya Singapore na Tanzania
kuanzisha biashara mpya zitakazowanufaisha wote.
Waziri Mkuu amesema Singapore ina
uwezo mkubwa kibiashara pamoja na uzoefu wa siku nyingi kwenye
uendeshaji wa bandari hivyo Tanzania itapata nafasi ya kujifunza namna
ya uendeshaji katika sekta hizo.
Amesema Tanzania imefungua
milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Singapore kuja kuwekeza
katika sekta za viwanda, usafiri wa anga na kwenye Maeneo ya Uzalishaji
kwa Mauzo Nje (EPZ).
0 maoni:
Chapisha Maoni