|
WAZIRI
Mkuu mstaafu, Joseph Warioba amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana (2015)
ulifanyika kwa haki huku akitaka vyama vya siasa kuwa na demokrasia
ndani yao, kuhakikisha wanayotaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
iwafanyie, wao pia wayafanye kwenye vyama vyao.
Amesema
nchi inatakiwa kuangalia na kujadili uchaguzi usiwe bidhaa inayotafutwa
kwa fedha kama ambavyo ilijitokeza katika uchaguzi wa mwaka jana ambao
rushwa ilitumika kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza
katika mdahalo wa kitaifa kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana,
Warioba pia ametoa angalizo kwa asasi za kiraia kuwa makini na wafadhili
wao kuepuka kuingiza matakwa yao (wafadhili) kwenye siasa za ndani.
Mdahalo
huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Mpango wa
Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu, (LHRC).
Akiwasilisha
mada, Warioba ambaye amepongeza utendaji wa Rais John Magufuli, alisema
uchaguzi mkuu ulikuwa na hamasa ambayo haijapata kutokea lakini ulikuwa
huru na ulimalizika kwa amani na utulivu .
Alisema
akiwa mmoja wa waangalizi aliyewahi kusimamia chaguzi za Zambia, Malawi,
Nigeria, Ghana, Ethiopia na Sudan, anafahamu masuala ya uangalizi na
kutoa ripoti. Alisema ni kweli uchaguzi ulienda vizuri. Alisema
alipoangalia maoni ya waangalizi wa nje alishangaa kwa mara ya kwanza
kusifu mchakato mzima wa uchaguzi.
Alisema
licha ya kuwapo kwa upungufu mdogo, waangalizi hao walisifu mchakato
mzima na zaidi alishangaa kuona waangalizi ambao wagumu kusifia ; mfano
Umoja wa Ulaya (EU), waliridhishwa na uchaguzi huo.
Vyama, asasi vyamulikwa
Hata
hivyo alisema, katika kukuza demokrasia kwenye vyama, yapo matatizo na
ipo kazi ya kufanya kwa kuwa rushwa imekuwa ikitumika kwa kuwepo
matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema bila kuleta demokrasia ndani ya chama, ni vigumu kufanikiwa katika kukuza demokrasia nchini.
“Ni
rahisi kulaumu Tume ya Uchaguzi (NEC) lakini ndani ya vyama hawafuati
yale wanayotaka NEC iwafanyie hivyo lazima kuwe na demokrasia ndani ya
chama kwani kukiwa na vyama bila demokrasia hatupati nchi yenye
demokrasia hivyo wanasiasa tupige kelele ndani ya vyama siyo
NEC,”alisisitiza.
Kwa
upande wa asasi za kiraia kuwa walifanya kazi ipasavyo lakini alishauri
elimu kwa mpigakura iwekwe kwenye mtaala wa shule nchini na isisubiri
kutolewa wakati wa uchaguzi.
Asasi na wafadhili
Akizungumzia
nafasi ya asasi za kiraia, alisema zipo baadhi katika kutoa elimu,
ziligeuka wanaharakati na kufikia kuhamasisha wachague chama au mgombea
yupi .
Alisema
walifanya hivyo ikidaiwa ni matakwa ya wafadhili jambo alilosema kwamba
ni hatari masharti ya wafadhili kuingilia siasa za nchi.
Wanahabari
Jaji
Warioba alizungumzia pia ushiriki wa vyombo vya habari katika uchaguzi
huo na kusema vyote vilikuwa na upendeleo. Alisema hata magazeti
yaliyosifika kwamba hayana upendeleo, yalizidi na mpaka sasa vyombo
hivyo vina upande wake.
Alitaja baadhi ya mambo ya kuboresha ni mfumo wa kisheria na kitaasisi kwa kuboresha katiba kukuza demokrasia.
Alisema
ushindi wa rais uhojiwe mahakamani na kuwepo kwa kura za uwiano kwa
wabunge kuleta usawa wa kijinsia pamoja na vyama vidogo vya siasa kukua.
NEC kulalamikiwa
Alisema lazima kuwa na tume inayoaminika na wote ambayo haitawekwa wanasiasa.
Akizungumzia
suala la gharama za uchaguzi,Warioba alisema sheria ipo lakini
haitekelezwi kwani vyama vikubwa vinapata faida kuliko vidogo .
Alisema uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa ni wa fedha hivyo kugeuka bidhaa kwa wenye fedha kushinda.
Alisema
athari zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu ni lugha iliyotumika ya
kukebehi ,kukejeli na matusi ikiunganishwa na ushabiki hali iliyoacha
makovu na uhasama katika jamii na miongoni mwa viongozi .
Alisema
kumekuwa na nyufa katika taifa kwa kuwepo rushwa na ubaguzi kwani rushwa
imekuwepo katika ngazi zote za mchakato wa uchaguzi kuanzia uteuzi wa
wagombea ndani ya vyama mpaka kutangaza matokeo.
Alisema
kumekuwa na ubaguzi wa kila aina ikiwemo ukabila, dini na kikanda ambao
nyuma ulijulikana kijiografia lakini sasa zinatumika kisiasa .
Alisema zipo nyufa mpya zinazoanza kujitokeza baina ya wazee na vijana.
Mdahalo
huo uliokuwa na kaulimbiu ya ‘Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania
mwaka 2015: Mchango wa waangalizi wa ndani kuelekea uchaguzi bora, huru
na haki’, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison
Mwakyembe.
Mwakyembe alisema takwimu za mwaka 2013-2014 zinaonesha kuwa kwa ujumla demokrasia nchini inazidi kuimarika na kushamiri.
Waziri
alisema inaonesha kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya 83 ikiwa na alama 50.5
kwa kukidhi vigezo vya demokrasia, ikilinganishwa na Kenya iliyochukua
nafasi ya 93 ikiwa na alama 48.1. Zambia ilichukua nafasi ya 94 alama
48.1; Nigeria nafasi ya 107, alama 40.6 na Afrika ya Kusini ikichukua
nafasi ya 71 alama 54.7.
0 maoni:
Chapisha Maoni