MIKOA ya Njombe, Iringa na Mbeya
imetajwa kuwa ndio mikoa yenye maambukizi makubwa zaidi ya Virusi vya
Ukimwi (VVU) nchini kutokana na kuwa na mwingiliano mkubwa wa watu
unaosababishwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa Tume
ya kudhibiti Ukimwi (Tacaids) Mkoa wa Mbeya, Edwin Mweleka, wakati
alipokuwa Mgeni Rasmi kwenye utambulisho wa Mradi wa ushirikishaji wa
wananchi wanaoishi na virusi vya Ukimwi wa ‘Sauti yetu’ unaofadhiriwa na
wananchi wa Marekani kuipitia Shirika la USAID.
Mweleka alisema kuwa Mkoa wa Njombe ndio
unaoongoza na kwamba maambukizi yamefikia asilimia 14.8, ukifuatiwa na
Iringa wenye asilimia 9.1 na Mbeya unashika nafasi ya tatu ukiwa na
asilimia 9, ambapo alisema kuwa mradi huo wa ‘Sauti yetu’ utasaidia
kupunguza maambukizi hayo.
“Tunashukuru wenzetu wa Marekani kwa
kutusaidia kufadhili Mradi huu wa Sauti yetu kupitia shirika lao la
USAID, na naamini kwa mikoa yetu hii yenye maambukizi makubwa mradi huu
utakuwa msaada mkubwa katika kupunguza maambukizi,” alisema.
“Mikoa ya ukanda wetu wa Nyanda za Juu
Kusini ndiyo inayooongoza kwa maambukizi ikiongozwa na Njombe ambao ndio
mkoa ambao unaongoza kitaifa wenye asilimia 14.8 ukifuatiwa na Iringa
wenye asilimia9.1 huku Mbeya tukishika nafasi ya tatu kwa asilimia 9,
hivyo kampeni itakayokuwa inaendeshwa kupitia ‘Sauti yetu’ tunatarajia
itusaidie kupunguza maambukizi hayo mpaka kufikia Sifuri Tatu,”
alisisitiza Mweleka.
Mweleka alisema kuwa mikoa ya Mbeya na
Iringa haijawahi kutoka kwenye orodha ya mikoa mitatu yenye maambukizi
makubwa tangu tafiti zilipoanza kufanyika katika miaka ya 2003/2004.
Mwenyekiti wa Baraza la Watu wanaoishi
na Virusi vya Ukimwi Nchini, Justine Mwinuka, alisema kuwa mradi huo
unatekelezwa katika Halmashauri 46 zilizopewa kipaumbele nchi nzima huku
katika Mkoa wa Mbeya zikihusika Halmashauri tatu ambazo ni Mbeya Jiji,
Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Alisema kuwa watu wanaolengwa kwenye
mradi huo ni wale wanaoishi na VVU pamoja na wenye TB kwa madai kuwa
magonjwa hayo yana uhusiano wa moja kwa moja.
Alisema kuwa Mradi huu unatambulishwa
kwa waratibu wa Ukimwi shughuli za Ukimwi ngazi ya Halmashauri pamoja na
watendaji wa mabaraza ya watu wanaoishi na VVU Ngazi za Wilaya (Konga)
Kwa upande wake Meneja wa Mradi huo wa
‘Sauti Yetu’, Rachel Jacob, alisema kuwa changamoto inayowakumba watu
wanaoishi na VVU kwa sasa ni unyanyapaa binafsi hali ambayo huwafanya
watu hao kuishi kwa wasiwasi wakati wote.
Alisema lengo kubwa la mradi huo ni
kutoa hamasa kwa jamii kupima afya zao kuanzia ngazi ya familia mpaka
Taifa ili kila mtu aweze kuijua afya yake na wale wanaokutwa na
maambukizi waweze kuanzishiwa dawa.
Jacob alisema kuwa Mradi huo ulianza kutekelezwa tangu mwezi Oktoba 2015 na utakamilika mwezi Oktoba mwaka 2019.
0 maoni:
Chapisha Maoni