Serikali  imeanza taratibu za ujenzi wa vituo vya ukaguzi wa magari makubwa  katika ukanda wa kati na ukanda wa Dar es Salaam ili kurahisisha biashara na usafirishaji wa magari makubwa yanayosafiri nje ya nchi.
Vituo vitakavyojengwa katika ukanda wa kati ni Vigwaza (Pwani), Manyoni (Singida) na Nyakanazi (Kagera) na kwa upande wa ukanda wa Dar es Salaam ni Vigwaza (Pwani), Mikumi (Morogoro), Makambako (Njombe) na Mpemba (Songwe).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Joseph Nyamhanga alisema hatua ya  ujenzi wa vituo hivyo ni kutekeleza  agizo la Rais, Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa mapema mwezi Aprili  mwaka huu wakati wa ufunguzi wa Daraja la Rusumo.
2
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga, akitoa ufafanuzi kuhusu stika za upimaji uzito katika mizani kwa magari makubwa yanayosafiri kwenda nje ya nchi. (Picha na Lorietha Laurence – Maelezo)

Mhandisi Nyamhanga  aliongeza kuwa vituo hivyo vya pamoja vitakuwa na huduma muhimu ikiwemo mizani, vituo vya polisi, vituo vya Mamlaka ya Mapato(TRA) na sehemu za mapumziko kwa madereva.
“Mizani hii ya pamoja ni kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji na biashara baina ya Tanzania na nchi za jirani pamoja na kupunguza msongamano wa magari  katika maeneo ya mizani” alisema Mhandisi Nyamhanga.
Kwa mujibu wa Nyamhanga alisema wakati  maandalizi ya  ujenzi wa vituo hivyo ukiendelea magari makubwa yanayosafiri kupitia ukanda wa kati kwenda nje ya nchi yatapimwa uzito katika vituo vya mizani vya Vigwaza (Pwani), Njuki (Singida) na Nyakahura (Kagera).
Aidha Nyamhanga alisema magari yanayosafiri kwenda nje ya nchi kupitia ukanda wa Dar es Salaam yatapimwa uzito wake katika vituo vya  Vigwaza (Pwani), Mikumi (Morogoro), Makambako (Njombe) na Mpemba (Songwe).
Mhandisi Nyamhanga pia aliieleza kuwa magari hayo yatakuwa na sticker maalum ili kutofautisha na yale yanayofanya safari za ndani ya nchi, ambazo zitauzwa kiasi cha dola 20 za kimarekani.
Vituo vilivyopo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani za Kenya, Uganda na Kongo ni Holili/Taveta mpakani mwa Tanzania na Kenya mkoani Kilimanjaro, Namanga Mkoani Arusha na Horohoro/Lunga mkoani Tanga na vingine ni Sirari/Isebania mkoani Mara, Mutukula mkoani Kagera,Rusumo mkoani Kagera na Kabanga/Kobero mkoani Kagera.
Na Lorietha Laurence – Maelezo