Jumapili, 24 Aprili 2016

MKAAZI WA WILAYA YA MICHEWENI PEMBA BAKAR HAJI FAKI (20) AMEJINYONGA NDANI YA NYUMBA YAKE ANAYOISHI .

imagesNa Masanja Mabula –Pemba
………………………………………….
MKAAZI wa kijiji cha Chamboni Shehia ya  Wilaya ya Micheweni Pemba  Bakar  Haji  Faki  (20)  amekutwa akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ndani ya nyumba yake anayoishi .
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema limetokea usiku wa Jumatano majira ya saa tatu , ambapo walimkuta akiwa amejitundika na tayari amefariki dunia .
Ali Massoud Kombo Mkaazi wa Micheweni aliliambia Gazeti hili kwamba tukio limeshangaza wengi kwani kabla ya kifo hicho kijana huyo hakuwahi kusumbuliwa  na chembe za ugonjwa .
“Ni tukio ambalo limetushangaza vijana  wengi  ,kwani kijana mwenzetu  hakukuwa na taarifa yoyote ya kusumbuliwa na ugonjwa wowote  ”alifahamisha Ali Massoud Kombo .
Naye Kai Daud  akizungumzia kifo hicho alisema kwamba kiliwashitua kwani kabla ya kutokea walikuwa pamoja  na marehemu katika vijiwe /maskani zao wakijadili masuala ya kujipatia kipato .
Alisema kimetokea hatuna budi kushukuru kwani itakuwa  ni mipango ya Mungu , kilicho baki na kumuombea mwenzetu ambaye tayari ametutangulia .
Tukio hilo pia limethibitishwa na kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Kamshina Msaidizi Mwandamizi Hassan Nassir Ali na kusema kwamba uchunguzi  bado unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho .
Alisema kwamba uchunguzi wa awali umethibitisha kwamba kijana huyo  amefariki kwa kijitundika ndani ya nyumba (geto)  yake ya kuishi  na alionekana na jamaa zake akiwa tayari amefariki dunia .
“Ni kweli hili tukio limetokea na jeshi la Polisi bado linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini hasa nini chanzo cha kifo hicho , lakini uchunguzi wa awali umebaini kwamba amejinyonga kwa kutumia kamba ”alifahamisha.
Hata hivyo kamanda Nassir alisema ni vyema wananchi kujenga utaratibu wa kutafuta ushauri juu ya mambo ambayo yanawatatiza , kwani sio vizuri kuchukua maamuzi ya kuidhulumu nafsi .

0 maoni:

Chapisha Maoni