Alhamisi, 28 Aprili 2016

HIVI NDIVYO HALI YA DAWA ZA KULEVYA NCHINI



Dawa za kulevya ni kemikali za asili (za kulimwa) au za kutengenezwa viwandani ambazo zina uwezo wa haraka wa kuathiri utendaji kazi wa asili wa mwili, akili na  tabia za mtumiaji pale zinapotumika vibaya. (rapid  physical, mental and behavioral change).
    Dawa za kulevya zinaweza kugawanywa katika Makundi Matatu:
    VILETA NJOZI/MARUWERUWE (Hallucinogens)
              (psychological dependence),
    VIPUMBAZA (Depressants) have both (psychological and physiological dependence)
    VICHANGAMSHI       (Stimulants) (psychological dependence)
    NB: Pia kuna dawa za tiba zenye madhara ya kulevya
          
Nchi yetu inakabiliwa na tatizo la matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya. Hali hii inachangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo uelewa mdogo wa jamii juu ya tatizo hili, mmomonyoko wa maadili na tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka.   
Urefu wa mpaka wa nchi wenye vipenyo vingi hurahisisha usafirishaji haramu wa  dawa za kulevya na kufanya udhibiti kuwa mgumu. Vilevile,  bandari zetu hutumiwa na baadhi ya nchi jirani kupitisha bidhaa zao hivyo kuwepo uwezekano wa nchi yetu kutumika kupitishia dawa hizo. 
Madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya  yanadhihirishwa katika nyanja mbalimbali zikiwemo za  kiuchumi, kiafya, kijamii, kisiasa, kiusalama na kimazingira.
Biashara ya dawa za kulevya husababisha mzunguko wa fedha haramu unaochangia kuongezeka  kwa mfumuko wa bei,  kuhodhiwa kwa uchumi na watu wachache, ongezeko la pengo la vipato na kuwepo kwa uwekezaji haramu. Aidha, matumizi ya dawa za kulevya hudhoofisha afya ya watumiaji na kuathiri uwezo wao wa kufanya kazi.
Badala ya Taifa kuelekeza rasilimali zake katika kukuza uchumi wa nchi, sehemu ya rasilimali hizi hutumika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya kama vile  kutibu watumiaji na kudhibiti wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Biashara ya dawa za kulevya huchangia kuvuruga mfumo wa maisha katika jamii ikiwemo kumomonyoka kwa maadili, biashara ya ngono, kudharaulika kwa tamaduni za jamii,  rushwa,   kushuka kwa kiwango cha elimu, utoro mashuleni na kazini na migogoro ya kijamii na kifamilia ambayo huchangia  kuvunjika kwa ndoa na ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira magumu. 
Matumizi ya dawa za kulevya hudhoofisha afya ya mtumiaji na kusababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo  homa ya ini, kifua kikuu na VVU/UKIMWI hasa kwa watumiaji kwa njia ya kujidunga  na vifo vya ghafla.
Wafanyabiashara wa dawa za kulevya huweza hujiingiza katika siasa na kushika nyadhifa ambazo ni nyeti serikalini ili kulinda na kuendeleza biashara yao. Pia wanaweza kufadhili chaguzi na kuwaweka madarakani vibaraka wao ili watekeleze matakwa yao.
 
 
Biashara ya dawa za kulevya huweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, ugaidi, uharamia na mapinduzi ya tawala halali zilizopo madarakani. Madhara mengine ni pamoja na ujambazi, utapeli, wizi na utekaji nyara.
Uharibifu wa mazingira unaotokana na dawa za kulevya unasababishwa na ukataji na uchomaji ovyo wa misitu na mapori ili kupata maeneo yaliyojificha kwa ajili ya kilimo haramu cha bangi. Kwa mfano, kuharibiwa kwa misitu ya Tao la Mashariki katika wilaya za Korogwe, Kilindi, Morogoro na Kilombero ili kulima bangi kumesababisha mmomonyoko mkubwa wa udongo na baadhi ya mito kukauka. Aidha, athari nyingine ni kutupwa ovyo kwa sindano zilizotumika mitaani na katika mwambao wa Pwani kama vile maeneo ya  Msasani, Mbudya na Bongoyo. 
Katika kipindi cha mwezi February mwaka 2014 kiasi cha kilo 239.5 karibia kilo 240 za heroin kilikamatwa katika miji ya Dar Es Salaam na Zanzibar kikiwahusisha watuhumiwa 13 kati yao wairani 8, Pakistan 4,  na Mgiriki moja. Njia inayotumika zaidi ni njia ya maji kupitia bandari na fukwe za pwani ya Tanzania zikiwemo za mikoa ya Tanga, Pwani, Dar Es Salaam, Lindi na Mtwara. 
Aidha, njia ya anga ambapo wasafirishaji humeza au  kuficha kwenye mabegi ya nguo na mbinu zingine za ufichaji wa dawa hizo umeendelea kutumika ili kuweza kukwepa vyombo vya dola wakati wa kusafirisha dawa hizo.
Taarifa zilizotolewa na vyombo mbalimbali vya kimataifa hasa Interpol na  UNODC jumla ya kilo 350 za heroin zilikamatwa na vikosi vya Wanamaji (Combined Maritime Forces (CMF)) wa Australia katika bahari kuu  ya Hindi pamoja kilo 265 za heroin zilikamatwa na vikosi vya wanamaji wa Canada (Combined Maritime Forces (CMF)) katika bahari kuu ya Hindi zikielekea Tanzania.
Katika kipindi cha mwezi Machi mwaka 2014 kiasi cha kilo 8.81867 za dawa za kulevya zikiwemo kilo 3 za Heroin na Cocaine kilo 5.81867 zilikamatwa zikihusisha watuhumiwa 4 kati yao wanawake wawili na wanaume wawili moja akiwa ni raia wa Marekani. Aidha, zilikamatwa kilo 4.18 za kemikali bashirifu aina ya ephedrine zikisafirishwa kwenda Afrika Kusini .   Katika kipindi hiki cha mwezi Machi njia ya anga imetumika zaidi kusafirisha dawa hizo. Mbinu zinazotumika kuficha dawa hizo ni kumeza na kuficha kwenye mabegi ya kusafiria.
 
 
Hii inamaanisha kuwa karibia tani 2.5 za heroin zilikamatwa na vikosi mbalimbali vya wamamaji ( Combined Maritime Forces) wanaofanya doria katika  Bahari Kuu (International Waters) ya Hindi zilizokuwa ziingizwe katika Nchi za Afrika ya Mashariki hasa Tanzania na Kenya ili zihifadhiwe, zichakachuliwe, zifungwe, ziuzwe na nyingine zisafirishwe tena kwa njia mbalimbali za kificho kupelekwa katika masoko ya Afrika Kusini, Ulaya, China na Marekani.
Hali kadhalika, zimekuwepo jitihada za kupunguza matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa watumiaji wa dawa hizo ikiwemo utoaji wa huduma  za tiba . Kwa mfano,  mwaka 2011 watumiaji 3173 katika Jiji la Dar Es Salaam  walipatiwa tiba, Jiji la Tanga walitibiwa watumiaji 739, Jiji la Mwanza 80, Manispaa ya Dodoma 345, Manispaa ya Morogoro 250 na Zanzibar 97.  Mwaka 2012, utoaji tiba ulikuwa kama ifuatavyo:- Jiji la Tanga watumiaji 836,  Tabora 130, Jiji la Mwanza 422, na Iringa watumiaji 43.
Elimu juu ya athari  za dawa za kulevya hutolewa  kwa umma  kupitia matukio maalum ya kitaifa yakiwemo Wiki ya Vijana, Sabasaba, Nanenane  na Siku ya UKIMWI  Duniani.   
Pia, elimu hii hutolewa  kupitia vyombo vya habari kama vile redio, luninga na magazeti.  Aidha, machapisho mbalimbali yanayohusiana na  dawa za kulevya husambazwa nchini  kwa lengo la kutoa elimu.
Kuna aina mbalimbali za tiba ambazo mtumiaji wa dawa za kulevya anaweza kuzipata ili atengema.
Ushauri nasaha unatumika zaidi katika hatua mbalimbali za tiba aidha kwa kutumia hatua kumi na mbili (Recovery Oriented System of Care) ambapo watumiaji hukaa kwenye nyumba za upataji nafuu ( Sober Houses).
Kuna dawa mbalimbali zinatumika ili kumpunguzia mtumiaji uteja na usugu katika hospitali mbalimbali za afya ya akili na dawa za kulevya (detoxification).      Tiba mpya nchini na kusini mwa jangwa la sahari ni ya methadone kwa watumiaji wa heroin. 
M apambano dhidi ya dawa za kulevya yanakabiliwa na matatizo na changamoto mbalimbali zikiwemo:- kushamiri kwa kilimo cha bangi ambacho  hufanyika katika maeneo yasiyofikika kiurahisi; kuwepo kwa mipaka mingi, ukanda mrefu wa pwani na njia zisizo rasmi katika mipaka ya nchi yetu hali inayorahisisha uingizaji wa dawa za kulevya nchini;  uhaba wa vyombo vya udhibiti wa dawa za kulevya baharini ambayo ni njia kuu inayotumika kuingiza viwango vikubwa vya dawa hizo nchini; wananchi kutoshiriki kikamilifu katika vita dhidi ya dawa za kulevya  kutokana na sababu mbali mbali kama vile hofu ya kudhuriwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya na uelewa mdogo wa tatizo hili.  
Changamoto nyingine ni:- ukosefu wa tafiti za kutosha kuhusu matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini; upungufu wa rasilimali za kupambana na tatizo la dawa za kulevya; uchache wa wataalamu katika kupambana na tatizo la  dawa za kulevya; unyanyapaa kwa watumiaji wa dawa za kulevya; kubadilika mara kwa  mara kwa mbinu na  njia za usafirishaji na ufichaji wa dawa hizo.
Jitihada nyingine ni pamoja na kutungwa kwa sheria mpya itakayoziba mianya yote iliyopo hivyo kusaidia udhibiti wa tatizo la dawa za kulevya nchini.
Kuuundwa kwa mamlaka/ chombo kipya huru na chenye nguvu kitakacho leta tija katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya 
Kuanzisha kwa vituo vya tiba vya methadone ikianza na manispaa za Jiji la Dar es Salaam na baadae katika maeneo mengine ya nchi yetu hasa meneo mengine hasa Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Tanga na Zanzibar. 
Kukuza uelewa kwa umma juu ya madhara ya dawa za kulevya hasa kwa vijana wa rika mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuingiza suala la dawa za kulevya katika mitaala ya elimu katika ngazi zote.
Kushirikisha jamii kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuwalinda watoa taarifa wanaofichua siri za wahalifu wa dawa za kulevya

0 maoni:

Chapisha Maoni