RAIS
John Magufuli amekamilisha kutengeneza muundo wa serikali yake na
anatarajiwa kutangaza muundo huo katika Gazeti la Serikali (GN) muda
wowote kuanzia sasa.
Kutokana
na kukamilika kwa muundo huo, Rais ameshatoa maelekezo ya utendaji kwa
mawaziri wote na viongozi wengine kulingana na muundo wa serikali yake
na hivyo wanatekeleza majukumu yao kutokana na maelekezo ya Rais.
Hayo
yalisemwa bungeni mjini hapa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
alipokuwa anatoa majumuisho ya hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu
kwa mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017.
Waziri
Mkuu alisema baada ya kuapishwa, Rais alianza kazi ya kuunda serikali
yake kwa kuteua mawaziri, makatibu wakuu na watendaji wengine, kazi
aliyoendelea kuifanya hadi hivi Aprili 20, mwaka huu alipoikamilisha.
Alisema
tofauti na magazeti la kawaida, GN hutolewa baada ya kukamilika
kujengwa kwa hoja juu ya suala husika na ndio maana isingekuwa vema kwa
Rais kutoa tangazo hilo wakati akiendelea kuunda serikali yake.
“Napenda
sasa kuliarifu Bunge kuwa Rais atatangaza kwenye GN muundo wa serikali
yake wakati wowote kuanzia sasa, na kwa maana hiyo Mawaziri wote na
viongozi wengine wa juu wa serikali wanafanya kazi kwa maelekezo ya
Rais, lakini pia kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema
Waziri Mkuu Majaliwa.
Hoja
kwamba serikali iliyopo madarakani haipo kihalali kutokana na
kutotangazwa kwa muundo wa serikali katika Gazeti la Serikali,
iliibuliwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman
Mbowe, na kusema ni moja ya sababu zilizoifanya kambi hiyo kususa hotuba
hiyo ya Waziri Mkuu.
Bunge
jana lilipitisha bajeti hiyo ya Waziri Mkuu, huku wabunge 93 wakiwa
wamepata nafasi ya kuijadili, wabunge 80 wakichangia kwa maneno bungeni,
na wengine 13 wakiwa wamechangia kwa maandishi.
Kabla
ya kujibu hoja zilizojitokeza kwenye mjadala wa hotuba yake, Waziri
Mkuu Majaliwa alitoa pole kwa wananchi waliokumbwa na maafa ya mafuriko
katika wilaya za Rombo, Moshi Vijijini na Kilosa.
|
0 maoni:
Chapisha Maoni