Jumla ya wahalifu 71 wamekamatwa ndani ya
siku 7 katika maeneo mbalimbali katika Kata ya Gongo la mboto,Wilaya ya
Ilala, Jijini Dar es Salaam wakiwa na kete za bangi pamoja na madumu ya
pombe aina ya gongo.
Idadi hiyo imetajwa leo Jijini Dar es salaam
na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa polisi, Bw. Lucas Mkongya alipokua
akifafanua juu ya malalamiko ya wananchi wa Gongo la Mboto kuhusu
uhalifu uliokithiri katika maeneo hayo pamoja na jitihada
wanazozichukua katika kuzuia uhalifu huo.
“Kweli uhalifu upo na kila siku tunajitahidi
kufuatilia maeneo yote ya Gongo la Mboto. ndani ya siku saba kuanzia
Aprili 14 hadi 20 mwaka huu tumekamata jumla ya kete za bangi 640 pamoja
na lita 90 za pombe aina ya gongo”alisema Kamishna Msaidizi Mkongya.
Kamishna Msaidizi Mkongya amesisitiza
wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za wahalifu
pia amewaomba wananchi wajitahidi kuunda ulinzi shirikishi utakaosaidia
kulinda maeneo yao kwa sababu polisi pekee hawawezi kulinda kila
nyumba.
Aidha, Kamishna Msaidizi Mkongya ametoa rai
kwa wazazi kutoa malezi mazuri kwa watoto wao kwa kuwa asilimia kubwa ya
wezi wa maeneo hayo ni watoto wao wenyewe.
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na walinzi
shirikishi wanajitahidi kufanya doria kila siku katika maeneo mbalimbali
Jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa na
kuchukuliwa hatua stahiki.
0 maoni:
Chapisha Maoni