NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, amemuomba Mwenyekiti wa Kamati ya
Maandalizi ya Tamasha la Pasaka Alex Msama, kupeleka huduma hiyo katika
mikoa ya Kusini kwa sababu wanakosa huduma ya neno la Mungu.
Kampuni ya Msama huandaa Tamasha
la Krismasi linalotarajia kufanyika Desemba mwaka huu na Pasaka
linalotarajia kufanyika mwakani hapa nchini.
Majaliwa alisema kwa sasa tamasha
hilo limekuwa na nguvu kubwa ya kuhakikisha inahamasisha jamii katika
mambo mbalimbali hivyo ni wakati wa mikoa ya kusini kufaidika.
Alisema kuwa serikali yake
imejipanga kuhakikisha kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuona serikali
yake inawajali na kuwapenda hivyo taasisi kama Msama Promotions, sasa
inahitaji kujitanua na kufika mikoa mingi ya Tanzania.
Waziri Mkuu alisema kuwa amekuwa
akifuatilia namna Tamasha la Pasaka linavyojitahidi katika kuelimisha na
kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia hasa wajane na yatima hivyo na
mikoa kama Lindi na Mtwara nayo inahitaji huduma hiyo.
“Nimefarijika sana na namna
kampuni ya Msama Promotions chini ya Mkurugenzi wake, Alex Msama namna
inavyofanyakazi zake katika kutoa burudani na kuelimisha jamii kwa maana
hivyo ningependa kuwaunga mkono katika hilo,” alisema Majaliwa.
Alisema mikoa mingi ikiwamo Lindi
na Mtwara nayo inachangamoto nyingi hivyo wanahitaji ujumbe kama
unatolewa katika Tamasha la Pasaka kuhakikisha kila kitu kinakwenda
sawa.
“Kutoa misaada kwa yatima sio
kitu kidogo lakini kubwa ni namna kampuni ya Msama Promotions chini ya
Mkurugenzi wake Alex Msama, inavyofanyakazi zake kwa kufuata sheria
katika hili nawapongeza lakini kubwa ni kukumbuka mikoa ya Kusini nayo
inahitaji huduma hiyo.
Alisema kuwa kuna waimbaji wengi
wakubwa ambao kwa sasa wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano na Msama
lakini bado hawajawahi kufika katika mikoa ya kusini hivyo ni wakati
wake kuhakikisha nao wananufaika na tamasha hilo.
Majaliwa amemtaka Msama kuendelea na huduma hiyo kwani serikali iko tayari kutoa msaada wa hali na mali.
Aidha Mkurugenzi wa Msama
Promotions Alex Msama amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa na kusema kuwa
atajitahidi kuboresha na kuhakikisha wananchi wote wa Tanzania
wananufaika na huduma hiyo.
Msama amesema kuwa amesikia kilio
cha Waziri Mkuu nakusema kuwa kamati yake iko makini na inajipanga
kuhakikisha ombi hilo linafanyiwa kazi.
0 maoni:
Chapisha Maoni