Kaimu Meneja wa Idara ya Takwimu
za Ajira na Bei wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja akitoa
ufafanuzi kwa wahariri wa vyombo vya Habari kuhusu matokeo ya Utafiti
wa Watu wenye uwezo wa kufanya Kazi leo jijini Dar es salaam. Matokeo
hayo yataiwezesha Serikali kuangalia upya tija ya utendaji kazi katika
shughuli zinazofanywa na makundi mbalimbali ili kubaini mchango wake
katika kukuza Pato la Taifa.Picha na Aron Msigwa –MAELEZO.
Baadhi ya Wahariri na Waandishi
wa Habari waliohudhuria ufafanuzi kwa wahariri wa vyombo vya Habari
kuhusu matokeo ya Utafiti wa Watu wenye uwezo wa kufanya 2014 Kazi leo
jijini Dar es salaam.
Baadhi ya wahariri wa vyombo
mbalimbali vya habari na waandishi wa habari wakisikiliza maelezo wakati
wa uwasilishaji wa matokeo hayo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa
kufanya kazi mwaka 2014.
…………………………………………………………………………………………..
Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)
imesema kuwa takwimu za matokeo ya utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa
Kufanya Kazi wa Mwaka 2014 zitatumika kufanya maboresho ya Mipango na
Sera mbalimbali za kukuza ajira na kupunguza umasikini nchini.
Matokeo ya utafiti huo yameonesha
kuwa asilimia 70.9 ya muda wa watu wenye umri wa miaka 15 au zaidi kwa
siku hutumika kwenye shughuli zisizo za uzalishaji ikilinganishwa na
asilimia 18.5 inayotumika kwenye shughuli za kiuchumi.
Akizungumza na wahariri wa vyombo
vya habari leo jijini Dar es salaam Kaimu Meneja wa Idara ya Takwimu za
Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja amesema kuwa matokeo hayo
yataiwezesha Serikali kuangalia upya tija ya utendaji kazi katika
shughuli zinazofanywa na makundi mbalimbali ili kubaini mchango wake
katika kukuza Pato la Taifa.
Amesema kwa mujibu wa utafiti
huo Tanzania ina nguvu kazi ya Taifa ya watu milioni 22.3 wanaume wakiwa
milioni 11 na wanawake wakiwa milioni 11.2 huku idadi ya watanzania
walio nje ya nguvu kazi ya Taifa wakifikia milioni 3.4.
Amefafanua kuwa idadi ya
watanzania walio kwenye ajira ni milioni 20 ikilinganishwa na watu
milioni 2.2 ambao hawako kwenye ajira huku akibainisha kwamba kiwango
cha nguvu kazi iliyo katika uzalishaji wa bidhaa na huduma za kiuchumi
na nguvu kazi iliyo tayari kujihusisha na uzalishaji mali kimepungua
kutoka asilimia 89.6 mwaka 2006 hadi asilimia 86.7 ya mwaka 2014.
Kwa mujibu wa utafiti amesema
kiwango cha watu wenye umri wa kufanya kazi walio na ajira kwa upande wa
wanaume kwa mwaka 2006 kilifikia asilimia 80.8 ikilinganishwa na
asilimia 82.1 za mwaka 2014 huku kiwango hicho hicho kwa upande wa
wanawake kwa mwaka 2014 kikifikia 73.8 kutoka 77.6 za mwaka 2006.
“ Kiwango cha watu wenye umri wa
kufanya kazi walio na ajira kwa ujumla kimepungua, hii inaonesha kuwa,
kiwango cha uchumi kuzalisha ajira kimepungua kidogo kutoka asilimia
79.2 mwaka 2006 hadi asilimia 77.8 mwaka 2014” Amesema.
Kuhusu masaa ya kufanya kwa watu
wenye umri wa miaka 15 na kuendelea Bi. Ruth Minja amesema kuwa kati ya
mwaka 2006 hadi 2014 kumekuwa na ongezeko la masaa ambayo watu hufanya
kazi kwa makundi yote ya ajira akifafanua kuwa watu wanaofanya kazi kwa
malipo na waliojiajiri wamekuwa wakifanya kazi zaidi ya saa 50 kwa wiki
kuliko hali nyingine za ajira.
“ Napenda kuwaeleza kuwa takwimu
hizi zitasaidia kuboresha sera ya ajira na programu nyingine ili kuwe na
uwiano kati ya saa za watu wanaofanya kazi, uzalishaji na malipo
wanayopewa” Amesisitiza.
Aidha, amefafanua kuwa kwa upande
wa ukosefu wa ajira kwa muda mrefu kwa watu wenye umri wa miaka 15 au
zaidi kote nchini wananwake wana kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira
kuliko wanaume kwa miaka yote ya utafiti uliofanywa na Ofisi hiyo toka
mwaka 2006 hadi 2014.
Amesisitiza kuwa ipo haja kwa
Serikali na wadau mbalimbali kushughulikia kiwango cha watu wasio na
kazi na wale ambao hawako tayari kufanya kazi yoyote ya kiuchumi
kutokana na ongezeko lake kuwa kubwa kutokana na athari yake kwa uchumi
wa taifa.
“ Kiashiria hiki katika utafiti
tulioufanya kinabainisha kuwa kiwango cha watu ambao hawakuwa na kazi
wala hawakuwa tayari kufanya kazi yoyote ya kiuchumi kimeongezeka kutoka
ailimia 10.4 za mwaka 2006 hadi 17.2 za mwaka 2014 “ Amesisitiza.
Ameeleza kuwa kufuatia kiashiria
hicho wanawake wana kiwango kikubwa zaidi kuliko wanaume kwa kuwa wao
hujishughulisha na shughuli za nyumbani ambazo sio za kiuchumi zikiwemo
za kufua nguo, kupika na malezi ya watoto.
0 maoni:
Chapisha Maoni