Coastal
Union imepoteza mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya
Yanga baada ya washabiki wake kuwa chanzo cha Mwamuzi kuvunja mchezo huo
uliofanyika Aprili 24, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya
Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana
leo (Aprili 27, 2016) jijini Dar es Salaam kwa kuzingatia Kanuni ya
28(2) ya Kombe la Shirikisho. Wakati mechi hiyo inavunjwa, Yanga ilikuwa
ikiongoza kwa mabao 2-1.
Pia Coastal Union imepigwa faini
ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kuzingatia Kanuni ya 42(26) ya Ligi
Kuu kutokana na vitendo vya vurugu za washabiki wake wakati wa mechi
hiyo. Pia TFF haitasita kufungiwa uwanja huo iwapo vitendo hivyo vya
vurugu za washabiki havitakoma.
Mwamuzi wa mchezo huo Abdallah
Kambuzi amefungiwa mwaka mmoja wakati Mwamuzi Msaidizi namba mbili
Charles Simon ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi. Adhabu hizo
zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.
Mchezaji Adeyum Ahmed wa Coastal
Union anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi
kutokana na kitendo chake cha kumpiga kichwa Mwamuzi wa Akiba baada ya
kutolewa nje. Hata hivyo, Ahmed hakufanikiwa kutimiza azma hiyo baada ya
Mwamuzi huyo kumkwepa.
Yanga imepigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kutokana
na kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho.
Vilevile malalamiko ya Coastal
Union kutaka mechi hiyo irudiwe yametupwa baada ya Kamati ya Mashindano
kubaini kuwa hayana msingi wowote.
0 maoni:
Chapisha Maoni