Kaimu Mwenyekiti Mtendaji wa
kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na
Pan African Power Solutions (T) Limited Bwn. Joseph O. R. Makandege
(katikati), akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusu taarifa ya upotoshaji iliyochapishwa na gazeti la
MwanaHALISI ikihusisha IPTL kutoa rushwa kwa viongozi waandamizi wa
ikulu na watendaji waandamizi wengine serikalini. Kulia ni Mkurugenzi wa
uendeshaji wa IPTL Bwn. Parthiban Chandrasakaran na kushoto ni msaidizi
wa mwenyekiti mtendaji Bwn. Rajiv Bhesania. Picha na mpiga picha wetu.
……………………………………………………………………………………………..
Makampuni ya kufua umeme ya
Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan Africa Power Solutions
(T) Limited (PAP), tumesononeshwa sana na taarifa iliyochapishwa na
gazeti la kila wiki la MwanaHALISI katika toleo namba 332 la tarehe 28 Machi 2016 lenye kichwa cha habari, “Siri za Kikwete, IPTL zafichuka ”; iliyoambatana na nukuu katika ukurasa wake wa mbele inayosomeka “…hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga alitembeza mlungula.
Taarifa hiyo iliyojaa uongo
pamoja na kashfa nzito ya rushwa kwa IPTL/PAP na kwa viongozi waandamizi
wa serikali ya awamu ya nne na wengine ambao bado wamo katika serikali
hii ya awamu ya tano, imediriki kudai kwa kunukuu maneno yafuatayo,….. “Sethi
alitoa rushwa kila mahali, ikiwamo Ikulu, ili kufanikisha mpango wake
huo….Alihonga kila mtu. Alitoa rushwa kwa kila aliyeona faili la Escrow.
Hadi maofisa wa Ikulu na viongozi waandamizi kutoka wizara ya
fedha……..hadi ndani ya jumba jeupe (Ikulu kwenyewe), Singasinga
alitembeza mlungula. Ni BoT pekee, ambako hakuhonga au kuombwa rushwa.”
Tungependa kukanusha taarifa hizi
za shutuma ya rushwa ambazo ni za uongo na uzushi mtupu wenye lengo la
kuichafua IPTL na wamiliki wake akiwemo Mwenyekiti Mtendaji, Bw.
Harbinder Singh Sethi. Taarifa hizi zisizo na chembe ya ukweli ndani
yake zinalenga kuchafua sifa ya Ikulu ambayo ni taasisi nyeti hapa
nchini kwa kuihusisha na upokeaji rushwa ambayo ni kosa la jinai kwa
mujibu wa katiba na sheria za nchi yetu.
Isitoshe taarifa hizi zimejaa
habari za uongo zilizobuniwa kwa nia na madhumuni maovu ya kuichafua
sifa za kampuni za IPTL/PAP na mwenyekiti wake Bw. Harbinder Singh Sethi
pamoja na kuwachonganisha dhidi ya wananchi wa Tanzania kwa kuwahadaa
na kuwaaminisha Watanzania kuwa IPTL/PAP inaendeshwa kwa misingi ya
rushwa na udanganyifu, hivyo basi haistahili kufanya biashara hapa
nchini.
Awali ya yote, tungependa
kuutarifu umma wa Watanzania kwamba tuhuma za rushwa ni tuhuma nzito na
wala siyo za kunyamaziwa kabisa. Rushwa ni moja kati ya makosa makubwa
ya kijinai ambayo vyombo vya dola vinatilia maanani sana. Hivyo basi,
kampuni ya IPTL/PAP haiwezi kukaa kimya wakati tuhuma kama hizi
zikiendelea kuchapishwa dhidi yake, huku ikiwahusisha viongozi
waandamizi wa serikali, bila ya gazeti husika pamoja na mwandishi wa
taarifa hizo kutoa udhibitisho wowote wa tuhuma hizo.
IPTL/PAP tunaamini kwamba
taratibu zote za kukabidhiwa kampuni ya IPTL (ikiwemo mali na madeni
halali) zilifuatwa. Tunaamini katika utawala wa sheria ambayo
inazingatia haki za kila mtu. Hivyo basi, haitakuwa busara kuendelea
kunyamazia vitendo vya kiovu vya kuichafua kampuni yetu vinavyofanywa na
baadhi ya vyombo vya habari kwa kisingizio cha “uhuru wa kutoa maoni” au “uhuru wa vyombo vya habari”. Kama
vyombo vya habari walivyo na uhuru wao, vivyo hivyo IPTL/PAP kama
kampuni ina uhuru wa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria za nchi
bila ya kubughudhiwa. Kwa kutuhumu IPTL/PAP au viongozi wake kutoa
rushwa, bila kuthibitisha, ni kuihujumu kampuni ili isiweze kutekeleza
majukumu yake ya kuchangia ukuwaji wa uchumi wa nchi yetu.
Joseph O. R. Makandege (ADVOCATE)
(Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria)
KAIMU MWENYEKITI MTENDAJI
Independent Power Tanzania Limited / Pan African Power Solutions (T) Limited.
(Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria)
KAIMU MWENYEKITI MTENDAJI
Independent Power Tanzania Limited / Pan African Power Solutions (T) Limited.
0 maoni:
Chapisha Maoni