MIKOA ya Dar es Salaam na Arusha
imeelezwa kuongoza kwa uchimbaji wa visima vya maji ya chini ya ardhi
usiozingatia sheria na kanuni za sera ya maji ya mwaka 2002 ambayo pia
imelalamikiwa na wadau kupitwa na wakati.
Akizungumza na wanahabari mjini Iringa
jana katika mkutano uliozungumzia mradi wa utafiti wa hali ya maji chini ya
ardhi, Mkurugenzi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji anayeshughulikia rasilimali
za maji, Hamza Sadick alisema baadhi ya watu katika mikoa hiyo na mingine yote
nchini wamekuwa wakichimba visima bila vibali.
Alisema pamoja na sera hiyo kulalamikiwa,
kwa kupitia sheria namba 11 ya mwaka 2009 ya usimamizi wa raslimali za maji kuna
kanuni zinazozungumzia taratibu zinazopaswa kufuatwa ili mchakato mzima wa
kutafuta na kutumia maji ya ardhini usiwe na dosari.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo ni kosa
kwa mtu au taasisi kuchimba maji ya ardhini bila kibali au kampuni kufanya kazi
hiyo bila kuwa na leseni na kibali cha kazi hiyo.
“Nikiri kwamba kuna tatizo kubwa la
kufuatilia utekelezaji wa kanuni na sheria hiyo. Udhaifu huo umewafanya baadhi
ya wadau wazalishe na kutumia maji ya ardhini bila kufuata taratibu
zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria hiyo,” alisema.
Mkuu wa mradi huo wa utafiti, Profesa
Japhet Kashaigili alisema ongezeko la matumizi ya maji ya chini ya ardhi nchini
limechochewa kwa kiwango kikubwa na kupungua kwa maji ya juu ya ardhi
kunakosababishwa na ongezeko la watu na shughuli za kibinadamu.
“Mradi huu wa utafiti utatuwezesha kujua
kiasi cha maji yaliyopo ardhini, sehemu yanapoingilia, yapo kiasi gani,
yanatosheleza watu kiasi gani na kwa muda gani,” alisema.
“Tusipokuwa makini, maji ya ardhini
yataathiriwa na shughuli za binadamu na kuongeza mgogoro wa maji nchini. Kuna
haja ya kufahamu namna visima vinavyochimbwa, vinavyojengwa na taratibu zingine
zote zitakazoyafanya maji hayo yawe ni kwa matumizi endelevu,” alisema.
Utakapokamilika, Profesa Kashaigili
alisema mradi huo wa miaka minne, ulioanza kutekelezwa mwaka jana, utasaidia
kukuza msingi, taratibu na usimamizi shirikishi kwa njia za kisayansi ambazo
rasilimali za maji ya chini ya ardhi zinaweza kutumika kwa uendelevu na hivyo
kupunguza umasikini katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa
Iringa Amina Masenza alisema kuna changamoto kubwa sana ya mgawanyo wa maji
jambo linalosababisha rasilimali hiyo isababishe migogoro katika maeneo
mbalimbali nchini.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba
yake na Mku wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, RC Masenza alisema mbali na
ongezeko la watu, shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi, kwa pamoja
yamesababisha upungufu wa maji.
0 maoni:
Chapisha Maoni