Naibu
Katibu Mkuu wa CCM, Rajabu Luhwavi akizungumza na viongozi na watumishi
wa CCM katika kikao chake maalum cha kuzungumza na wafanyakazi wa mkoa
wa Njombe kilichofanyika mjini Njombe. Kushoto ni Katibu wa CCM mkoawa
Ruvuma Verena Shumbusho na kulia ni Katibu wa CCM mkoa wa Njombe Osea
Mbagike.
………………………………………………………………………………………………..
Na Bashir Nkoromo,Njombe
Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kimesema, kina mpango wa kuhakikisha kila mtumishi wake anapatiwa huduma
ya Bima ya Afya ikiwa ni moja ya hatua ya kuboresha maisha ya watumishi
hao.
Kimesema kupitia mpango huo, kila mtumishi hadi wa ngazi za chini ataweza kupata matibabu yeye na familia yake nchini kote.
Ahadi hiyo ilitokewa jana na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Bara, Rajab Luhwavi alipokuwa akizungumza
na watumishi wa Chama na Jumuiya zake mkoani Njombe akiwa katika ziara
ya kikazi ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero na changamoto
zinazowakabili watumishi wa Chama.
Luhwavi alisema kwa sasa Chama
kimo katika jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kuwapatia huduma
hiyo ya bima ya afya watumishi wake ili wapate huduma ya matibabu kwa
urahisi badala ya kutaabika kupata matibabu waanapougua jambo ambalo
linawapunguzia ufanisi katika kazi.
Alisema, kwa sasa watumishi wengi
wa Chama hawawezi kuingizwa katika mpango huo wa bima ya afya kutokana
na vima vya mishahara yao kutokidhi viwango vinavyotakiwa ili kusajiliwa
na taasisi zinazotoa huduma hiyo ya bima ya afya hivyo chama
kikishapata fedha kitajazia mishara ya watumishi wenye vima vidogo ili
kila mmoja aweze kuwa na sifa za kusajiliwa.
Naibu Katibu Mkuu huyo, aliongeza
kwamba mpango huo utaanza kwa watumishi wa CCM na baadaye itakwenda hadi
kwa watumishi wa Jumuiya za chama ili nao wanufaike na utaratibu huo wa
bima ya afya.
“Nduguzangu siyo kwamba changamoto
zote hatuna uwezo wa kuzitatu, kwa kweli baadhi ya changamoto tuna
uwezo wa kuzitatua isipokuwa kinachotakiwa ni namna ya kujipanga tu,
hivyo nina uhakika jambo hili litawezekana”, alisema Luhwavi.
Katika hatua nyingine Chama cha
Mapinduzi kimesema ili kuhakikisha mpango wake wa kuendana na mabadiliko
ya sasa unafanikiwa haraka, kinasimamia viongozi wake kwa karibu zaidi
ili kuhakikisha kila mmoja anawajibika ipasavyo katika kuwahudumia
watumishi walio chini yake hasa wa ngazi za chini.
Akitoa kauli hiyo wakati
akizungumza na watumishi wa Chama mkoani Njombe, Luhwavi alisema,
alisema ni lazima chama kiwasimamie viongozi wake kwa makini kwa sababu
viongozi kutohudumia kwa haraka na kwa uadilifu mkubwa wafanyakazi ni
miongoni mwa vikwanzo vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wa haraka lengo
hilo la Chama kwendana na mabadiliko ya sasa.
“Tunajua wapo baadhi ya viongozi
wa Chama chetu ambao bado wanafanyakazi zao kwa mtindo wa kimangimeza
ikiwa ni pamoja na kutotoa ushirikiano watumishi walio chini yao
wanapohitaji ufumbuzi wa matatizo au changamoto zinazokuwa zinawakabili
kwa namna mbalimbali”, alisema Luhwavi.
Alisema, imefika wakati sasa
viongozi wa Chama kuacha tabia ya baadhi yao kufanya kazi kwa mazoea
badala yake wajikite katika kushirikiana na wananchi kwa karibu katika
kufanyakazi za kijamii kama ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu,
zahanati na miraji ya maji.
0 maoni:
Chapisha Maoni