…………………………………………………………………
Na Felix Mwagara, Misungwi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Misungwi mkoani Mwanza, Charles
Kitwanga amemtaka Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Misungwi
kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafukuza kazi wauguzi na madaktari
watakaokuwa wanawaomba rushwa wananchi jimboni kwake.
Kitwanga alisema amekuwa akipokea
malalamiko kutoka kwa wananchi kwa muda mrefu kuwa rushwa imekithiri
katika hospitali ya Wilaya jimboni humo na kuwakatisha tamaa wananchi
wanaoenda kupata huduma hospitalini hapo.
Akizungumza huku akishangiliwa na
mamia ya wananchi wa mjini Misungwi, Kitwanga alisema hali sasa imekuwa
tete hivyo lazima tuchukue hatua kali kwa wale watumishi wachache ambao
hawafuati sheria na kuweka mbele rushwa kwa wananchi.
“Ndugu wananchi madaktari na
wauguzi ni watu muhimu sana katika jamii kwani wanatupa huduma nzuri
kabisa, ila wataalamu hawa wanachafuliwa majina yao kwa watumishi
wachache mno, sasa tunataka kuwaondoa wale wachache ili tubaki na wengi
ambao wanaipenda kazi yao, nawaonya wale wachache wenye tabia hiyo
waiache haraka iwezekanavyo,” alisema Kitwanga.
Alifafanua kuwa ni kosa kwa
daktari au muuguzi kumuomba rushwa mgonjwa au ndugu wa mgonjwa, kufanya
hivyo ni hatari ni sawa na kuua, hivyo lazima sheria ifuate mkondo wake
ili kulimaliza tatizo hilo sugu ndani ya Hospitali ya Wilaya pamoja na
Misungwi kiujumla.
“Ndugu wananchi msiwe na wasiwasi
kabisa, nina aapa sitalivumilia tatizo hilo, na Mkurugenzi yupo hapa
analisikia hili, hivyo lazima alifanyie kazi kwa kuwasimamisha kazi
wauguzi au madaktari watakaotuhumiwa kuomba au kupokea rushwa,“ a;lisema
Kitwanga huku akishangiliwa na wananchi jimboni humo.
Wakati huohuo, Kitwanga aliwataka
wananchi hao kuanzisha vikundi ili waweze kupewa mikopo kupitia fedha
alizoziahidi Rais John Magufuli kuwa atatoa kwa kila kijiji shilingi
milioni hamsini.
“Fedha zipo jirani kuja, hivyo
anzisheni vikundi ili muweze kukopeshwa fedha hizo na muweze kufanya
mambo ya maendeleo, fedha hizo ni kwa ajili ya mikopo hivyo tumieni
fursa hiyo kwa kuanzisha vikundi vyenu ili muweze kuzipata fedha hizo
kwa uharaka zaidi,” alisema Kitwanga.
Hata hivyo, Waziri Kitwanga
aliwahakikishia wananchi wa jimbo hilo wawe watulivu na wasubiri
maendeleo, na pia waendelea kuchangia maendeleo ya jimbo lao ikiwemo
uchangiaji wa madawati katika shule zao. Kuhusu barabara Kitwanga
alisema barabara zote ambazo hazipitiki zitatengenezwa hivi karibuni na
tatizo la maji litakuwa historia kwani mipango ya upatikanaji wa maji
hayo ilishakamilika.






0 maoni:
Chapisha Maoni