Na Jonas Kamaleki, MAELEZO
Shilingi bilioni 374.5 zimetolewa
kwa ajili ya mikopo ya nyumba hapa nchini ili kuwawezesha wanachi kuwa
na makazi bora ambayo ni haki ya msingi ya kila mwanadamu.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William
Lukuvi wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani.
“Ili kukidhi mahitaji ya nyumba
yanayotokana na ongezeko kubwa la watu, Serikali kwa kushirikiana na
wadau mbalimbali imeshiriki katika utoaji wa mikopo ya nyumba ambapo
soko la mitaji na mikopo ya nyumba nchini limeongezeka na kufikia
asilimia 6.7 kwa mwaka jana,”alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi,
taarifa za Benki Kuu zinaonyesha kuwa idadi ya benki zinazotoa mikopo ya
nyumba zimeongezeka kutoka tano kwa mwaka 2010 hadi kufikia 26 Desemba
2015.
Aidha. Lukuvi amesema kuwa utoaji
wa mikopo ya muda mrefu ya nyumba umewezesha sekta binafsi na
waendelezaji milki kuingia katika biashara ya kujenga na kuuza nyumba za
biashara na makazi kwa kuwauzia wananchi kwa mkopo wa muda mrefu.
Aliongeza kuwa ili kuwezesha
sekta ya nyumba kuendelea kufanya vizuri, Serikali inafanya mapitio ya
sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya nyumba, zikiwemo Sera ya
Ardhi ya mwaka 1995 na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka
2000. Lengo la mapitio hayo ni kuweka mfumo wezeshi ambao utarahisisha
uendelezaji wa sekta hiyo.
Serikali kupitia Wakala wa Taifa
wa Utafiti wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) imesaidia kukuza
tekinolojia asilia ya vifaa vya ujenzi, kuhamasisha na kusambaza matokeo
ya utafiti na utaalam wa ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu,
alisema Lukuvi.
Lukuvi amebainisha kuwa katika
mwaka wa fedha ulioisha, Wakala ulitengeneza mashine 80 za kufyatulia
tofali za kufungamana ambapo kati ya hizo, mashine 46 ziliuzwa kwa
vikundi 12 vya ujenzi. Wakala pia ulitoa mafunzo ya ujenzi wa nyumba za
gharama nafuu kwa vikundi 110 katika wilaya za Kahama, Morogoro na
Kinondoni.
Waziri Lukuvi amesema kuwa
Shirika la Nyumba limeendela kutekelza miradi yake 64 yenye jumla ya
nyumba 4,990. Miradi hii imeliwezesha Shirika kufikia mikoa 24 kwa
kujenga nyumba za makazi ya gharama nafuu 1,841, gharama ya kati 2,823
na nyumba za biashara 326.
“Wizara yangu imekuwa
ikishirikiana na Mamlaka za Upangaji Miji katika uandaaji wa Mipango
Kabambe ya miji, Manispaa na Majiji, hadi kufikia Septemba 30, 2016
Rasimu za Mipango hiyo kwa Jiji la Mwanza, Manispaa za Mtwara,
Iringa,Tabora, na Musoma pamoja na Mji wa Kibaha zilikuwa zimekamilika
na kutangazwa kwenye gazeti la Habari Leo ili kuwawezesha wadau wa maendeleo kupitia rasimu na kutoa maoni yao,”alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi amesema pia kuwa
zoezi la urasimishaji makazi katika jiji la Dar es Salaam unaendelea
katika maeneo ya Kimara, Chasimba na Makongo Juu. Hadi kufikia Septemba
2016 viwanja 4,818 vilitambuliwa ambapo kati ya hivyo. Viwanja 4,665
vimepimwa na maandalizi ya umilikishaji yanaendelea.
Siku ya Makazi Duniani
huadhimishwa Jumatatu ya kwanza ya Oktoba kila mwaka ikiwa ni
utekelezaji wa Azimio Na 40/202 lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa mwezi Desemba 1985. Kwa mwaka huu Maadhimisho haya yana
kaulimbiu isemayo Nyumba Kitovu cha Miji (Housing at the Centre).
0 maoni:
Chapisha Maoni