Viongozi
na Wanachama wa Chama cha Mapinduzi {CCM } ngazi ya Matawi Nchini
wameagizwa kujipanga vyema ili kuhakikisha Viongozi watakaowachagua
wakati utakapowadia wa uchaguzi ndani ya chama hicho hapo mwakani wawe na
sifa sahihi zitakazokidhi mahitaji yote ya kuwatumikia wanachama hao
katika kipindi cha miaka Mitano ijayo.
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi
alitoa agizo hilo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati za Siasa za
Matawi ya Mangapwani na Mangapwani Bondeni katika mkutano wa kuwashukuru
wanachama hao baada ya kumalizika kwa uchaguzi Mkuu uliopita.
Balozi
Seif Ali Iddi ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda akiambatana
pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Bahati Ali Abeid na Madiwani wa Wadi
zilizomo ndani ya Jimbo hilo alisema CCM ikiendelea kujipanga vyema
kwenye chaguzi hizo itakuwa na uhakika wa kuendelea kuongoza Dola ya
Watanzania katika miaka mingi ijayo.
Alisema
wapo baadhi ya wapinzani walijipenyeza kwenye chaguzi za Chama hicho
mwaka 2012 na kuomba Uongozi wakitumia hila na ujanja wa fedha na
hatimae kuwayumbisha Viongozi na Wanachama wakati wa kupanga safu ya
utekelezaji wa Ilani na Sera za CCM.
Mjumbe
huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwapongeza Wana CCM na Wananchi wa
Mangapwani kwa uamuzi wao walioufanya mwezi Oktoba mwaka 2015 na Machi
2016 wa kuipa dhamana CCM iendelee kuongoza Dola ya Tanzania katika
chaguzi zote mbili ile ya Zanzibar na ya Tanzania.
Balozi
Seif alisema kazi inayowakabili Wananchi kwa hivi sasa ni kuelekeza
nguvu zao katika kuimarisha miradi ya Kiuchumi na Maendeleo na kwa
upande wa Uongozi wa Jimbo hilo tayari umeshajipanga kuhakikisha
changamoto zinazowakabili Wananchi wa Maeneo hayo zinapatiwa ufumbuzi
muwafaka.
Alisema
yeye pamoja na Mbunge wake Mh. Bahati watashirikiana na viongozi wa
Jimbo hilo ngazi ya Jimbo na Matawi katika ujenzi wa Jengo Jipya la
Ofisi ya CCM Tawi la Mangapwani Bondeni litakalolingana na hadhi ya
Chama chenyewe.
Balozi
Seif aliwahakikishia Viongozi na Wanachama wa CCM wa Tawi la Mangapwani
Bondeni kwamba yeye binafsi pamoja na Viongozi wenzake atasimamia
maandalizi ya kuanza kwa msingi wa ujenzi wa Jengo hilo ili kuondoa kiu
ya muda mrefu waliyokuwa nayo Wanachama hao.
Naye
Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mh. Bahati Ali Abeid aliwathibitishia
Wanachama na Viongozi wa Matawi hayo kwamba juhudi za awali zimeanza
kuchukuliwa katika mwanzo wa kuzitafutia ufumbuzi changamoto
zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.
Mh.
Bahati alisema katika utekelezaji wa ahadi, Ilani na Sera za Chama cha
Mapinduzi za kusimamia upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama kwa
wananchi wa Matawi hayo Uongozi wa Jimbo hilo umeanza harakati za
kuliondosha tatizo hilo sugu linalowakabili Wananchi hao.
Alisema
ulazaji wa mabomba ya maji katika mradi maalum ulioanzishwa
unatekelezwa katika Vijiji vya Kiomba Mvua, Fujoni na Mangapwani na
kilichobakia kwa wakati huu ni Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA }
kukamilisha uwekaji wa Mashine ya kusukumia Maji katika kisima
kilichochimbwa kwenye eneo hilo.
Mbunge
huyo wa Jimbo la Mahonda alifafanua zaidi kwamba juhudi hizo za
uimarishaji wa miundombinu katika Sekta ya Maji zimechukuliwa kwa
makusudi na Uongozi wa Jimbo hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji
Zanzibar baada ya kubaini kwamba Kisima kilichokuwa kikisambaza huduma
ya maji katika kijiji hicho kiliopo Mfenesini kuzidiwa mara dufu.
Akigusia
uhai wa Chama cha Mapinduzi Mh. Bahati aliwakumbusha Wanachama wa
Matawi hayo kuhakikisha wanalipa ada zao kama kawaida bila ya kusibiri
kusukumwa kufanya hivyo ili kukipa nguvu chama chao kiweze kutekeleza
majukumu yake kama kawaida.
Mapema
Mke wa Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya
Siasa la Wilaya ya Kaskazini “B” Mama Asha Suleiman Iddi waliwanasihi
Wazee wa Vijiji hivyo Kuanzisha Kamati ya maadili itakayosaidia kutoa
elimu kwa vijana waliojitumbukiza katika matumizi ya Dawa za kulevya.
Mama
Asha alisema inasikitisha kuona jitihada kubwa zilizochukuliwa na
Uongozi wa Jimbo hilo kwa kutumia fedha nyingi katika kuwapatia ushauri
nasaha vijana hao kwenye nyumba za kurekebisha tabia { Sober House }
hatimae ziligonga mwamba.
Alisema
Kamati itakayoundwa katika Kijiji hicho cha Mangapwani itapaswa kwenda
kujifunza kwa Kamati kama hiyo iliyoanzishwa katika Kijiji cha Fujoni
ambayo imeleta mafanikio makubwa katika kukabiliana na wimbi la vijana
waliojitumbukiza katika wimbi la matumizi ya dawa za kulevya.
Mama
Asha alieleza kwamba Vijana wa Fujoni walioamua kuacha dawa hizo tayari
hivi sasa wamekuwa na mafanikio makubwa katika muendelezo wa mradi wao
wa Uvuvi unaokidhi mahitaji yao ya kimaisha baada ya kupatiwa msaada wa
Boti pamoja na Mashine yake.
0 maoni:
Chapisha Maoni