Postedy by Esta Malibiche on August 3, 2016 in BIASHARA with No comments
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku moja kwa uongozi wa Manispaa ya
Morogoro kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo na
kuyatangaza kesho.
“Mbali na kutenga maeneo pia
nawaagiza muwasaidie wafanyabiashara hawa kuunda vikundi kulingana na
aina ya biashara wanazozifanya ili kuwawezesha kupata mikopo kwa urahisi
kutoka katika taasisi za fedha” alisema.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo leo
(Jumatano, Agosti 03, 2016) wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa
kituo cha mabasi Msamvu unaojengwa kwa ubia kati ya Manispaa ya Morogoro
na Mfuko wa Pensheni wa LAPF.
Awamu ya kwanza ya mradi huo
inatarajiwa kufunguliwa Agosti 12 mwaka huu utakuwa ni kituo cha mabasi
cha kwanza cha kisasa Tanzania ambapo Waziri Mkuu amezitaka halmashauri
zote zilizoko makao makuu ya mikoa nchini kuiga mfano huo.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kulipongeza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Morogoro na LAPF kwa
kubuni mradi huo wa kisasa utawezesha abiria kupata taarifa ya basi
lilipo na muda litakapowasili kituoni hapo hivyo kupunguza udanganyifu
kutoka kwa mawakala wasiokuwa waaminifu.
Kwa upande wake Meneja wa mradi
huo Stanley Mhapa alisema mradi huo umegharimu sh. bilioni 40 ambapo
Manispaa inamiliki asilimia 40 ya hisa na mfuko wa LAPF unamiliki
asilimia 60.
“Mafanikio ya mradi huu ni pamoja
na kuiwezesha Manispaa kuongeza ukusanyaji wa mapato kutoka sh 350,000
kwa siku hadi kufikia sh. milioni 1.7 kwa siku,” alisema.
Mhapa alisema mradi huo
utakapokamilika utatoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma za
kibenki, vibanda vya biashara, sehemu za chakula, ofisi na sehemu ya
mapumziko ya abiria na vibanda vya kukatia tiketi.
0 maoni:
Chapisha Maoni