Postedy by Esta Malibiche on August 28.2016 in News
Mkuu wa wilaya Ikungi, Miraji
Mtaturu, akikagua ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Kaugeri wilayani humo
ambayo mkandarasi ametoweka bila kukamilisha ujenzi.
…………………………………………………………………..
MKUU wa wilaya ya Ikungi mkoani
Singida, Miraji Mtaturu, ameamuru kuwekwa ndani kwa viongozi wanne wa
kijiji cha Kaugeri kilichopo katika wilaya hiyo kwa kosa la kuuza ardhi
bila ya kufuata kanuni na taratibu zilizopo.
Aidha ameagiza kutafutwa
mkandarasi Samweli John na kuwekwa rumande kutokana na kutokamilisha
ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho wakati alishalipwa shilingi milioni
19.
Akizungumza katika mkutano wa
hadhara kijijini hapo, Mtaturu amesema watendaji hao wamegawa ardhi kwa
mwekezaji zaidi ya hekta 150 na kuingia mikataba ya kiunyonyaji wakati
kisheria kijiji hakitakiwi kutoa ardhi zaidi ya hekta 50 hivyo wamewekwa
ndani mpaka jumatatu ili wahojiwe na kutoa maelezo na hatimaye maamuzi
yafuate.
Amewataja waliosekwa rumande kuwa
ni mwenyekiti wa kijiji cha Kaugeri Mange Nkuba, ,aliyekuwa kaimu
mtendaji wa kijiji, Laurent Komba, na wajumbe wawili wa serikali ya
kijiji, Paul Kilo na Aman Clement ambaye anaendelea kutafutwa baada ya
kutoroka kabla ya mkutano kufanyika.
Kuhusu ujenzi wa Zahanati hiyo ya
Kijiji hicho, Mtaturu amesema mkandarasi huyo alitoweka toka mwaka 2013
na hivyo kufanya ujenzi huo kusimama wakati fedha alishachukua.
Kadhalika, ametoa muda wa mwezi
mmoja kwa wananchi walio katika eneo la msitu uliotangazwa kuwa hifadhi
toka mwaka 2003 kuondoka wenyewe katika eneo hilo kabla hawajatolewa kwa
nguvu kutokana na kuharibu mazingira.
Amewaasa wananchi kushirikiana kwa
pamoja katika kutii maelekezo na maagizo yanayotolewa na serikali ili
kuifanya Ikungi isonge mbele kimaendeleo.
0 maoni:
Chapisha Maoni