Rais wa uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa shambulizi la bomu la kujitoa muhanga lililofanywa siku ya Jumamosi katika mji wa Gaziantep lilifanywa na mtu anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 12 na 14.
Erdogan amesema anaamini kuwa wapiganaji wa kundi la Islamic State huenda wakawa wametekeleza shambulizi hilo, ambalo limeuwa zaidi ya watu 50 waliokuwa kwenye harusi ya kikudishi.
Hili linatajwa kuwa ni shambulizi kubwa zaidi kutokea kwa mwaka huu nchini humo huku wapiganaji wa IS wamepoteza ardhi katika Jirani na Kaskazini mwa Syria.
Ripoti zinasema kuwa waasi wanaoisaidia Uturuki wanajiandaa kukabiliana nao katika mipaka kati ya nchi hizo mbili, huku Naibu Waziri Mkuu Mehmet Simsek amesema mlipuko huo ni kitendo cha kinyama huku akiongeza kuwa huenda lilitekelezwa na wapiganaji wa kujitoa muhanga.
Rais Erdogan ameongeza kuwa hakuna tofauti kati ya IS, Vuguvugu lililopigwa marufuku la PKK na wafuasi wa kiongozi wa kidini aliyeko uhamishoni nchini Marekani Fetullah Gulen ambaye alilaumiwa kwa kupanga jaribio la mapinduzi lililotibuka mwezi uliopita.
Na Derick Highiness