Mzee Said Maohamed Mannoro, Mkazi
wa wilaya ya Kilwa – Kivinje akitoa ufafanuzi kuhusu nafasi ya wazee na
mchango wao katika maendeleo ya Taifa.
……………………………………………………………………..
Na. Aron Msigwa – Dar es salaam
Watanzania hususan vijana
wametakiwa kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa
vitendo kwa kufanya kazi kwa bidi, kulinda na kudumisha amani iliyopo na
kufanya matendo yenye tija na manufaa kwa Taifa.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar
es salaam na Mzee Said Maohamed Mannoro, Mkazi wa wilaya ya Kilwa –
Kivinje wakati akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa
habari hii kuhusu nafasi ya wazee na mchango wao katika maendeleo ya
Taifa.
Amesema yeye kama mzee anao wajibu
wa kuwaeleza na kuwashauri vijana kuepuka kutumika kama chanzo cha
kufanya vitendo vinavyochochea vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani
iliyopo.
“Mahali ambapo panahatarisha amani
hakuna mjadala, suala la amani linapewa nafasi ya kwanza mambo mengine
yanafuata, hata kama kungekuwa na jambo zuri namna gani linalotaka
kufanyika linapohatarisha amani kwa upande mmoja au mwingine ni afadhali
kuliacha” Amesisitiza mzee Monnoro.
Amesema kuwa maandamano
yaliyopangwa kufanywa na baadhi ya vyama vya Siasa Septemba mosi hayana
sababu ya kufanyika kwa kuwa yana ajenda ya kukosa uvumilivu kuhusu
usahihi wa uongozi wa nchi hivyo ni vyema wananchi wakayaepuka kwa
kuendelea na shughuli zao za kujiingizia kipato kwa kuwa amani haina
mjadala.
Amesisitiza kuwa ni vyema viongozi
wa vyama vya hivyo wakatumia njia zinazostahili kutafuta ufumbuzi wa
kero zao kupitia mazungumzo ili kupata haki kuliko kuwahamasisha
wananchi kuandamana na kupambana na vyombo vya dola na jambo ambalo
mwisho wake ni kuleta vurugu zisizo na maana.
Aidha, amewaomba viongozi hao wawe
na busara na waheshimu maisha ya watu wanaowaongoza pia waepuke kuwa na
kiburi cha kujiona wao ni bora kuliko wanachama wao.
“Mimi nayezungumza hapa niko
upande wa upinzani, yanapokuja mambo ya kitaifa hayanizuii kuzungumza
kwa kuwa yana manufaa kwa taifa, nasema kiongozi yeyote anayewashawishi
wafuasi wake waandamane bila sababu za msingi ni kosa na jambo hili ni
kupungukiwa na busara” Amesema mzee Mannoro.
Amebainisha kuwa kiongozi
asiyeheshimu wala kujali maisha ya wananchi wake na kujiona anajua
kuliko wao hafai, anapoteza sifa za kuwa kiongozi akisisitiza kuwa
watanzania wanayo fursa nzuri ya kuchagua mustakabali mwema wa Taifa lao
kwa kuwa amani ya Tanzania haina mbadala.
Akifafanua kuhusu utendaji wa
viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali za Serikali kuanzia kijiji
hadi Taifa amesema kuwa katika nafasi zao wanao wajibu wa kulisaidia
Taifa kwa kuwa wasimamizi wa utekelezaji wa malengo yaliyopangwa.
“Sote tunafahamu Serikali imekuwa
ikitekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo suala la utoaji wa
elimu bure haya ndiyo mambo ya msingi ya kufuatilia na kusimamia kwa
kila kiongozi katika nafasi yake, tunapaswa kumsaidia Rais wetu
kutekeleza malengo yake” Amesisitiza.
Kuhusu maboresho ya sekta ya elimu
ameishauri Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuwekeza katika
miundombinu ya elimu hasa ujenzi wa madarasa na mabweni ili kuwawezesha
wanafunzi wanaokaa mbali na shule hususani eneo analotoka la wilaya ya
Kilwa Kivinje ili waweze kuondokana na tatizo la kutembea umbali mrefu.
Ametoa wito kwa watanzania
hususan vijana kujikita katika shughuli za kilimo na shughuli nyingine
zinazoweza kuwaongezea kipato badala ya kupoteza muda mwingi katika
masuala yasiyo na tija kwa maendeleo yao binafsi na taifa.
Amesisitiza kuwa Kilimo sio adhabu
kwa kuwa yeye mwenyewe pamoja na uzee wake shughuli za kilimo
zimemsaidia kujenga familia imara na kuendesha maisha yake akiamini kuwa
utajiri wa kweli uko kwenye ardhi.
“Kinachonigusa mimi ni maisha ya
watu, nawaomba watumishi wa Serikali waliosomea mambo ya kilimo wafanye
kazi kwa bidi, wawasimamie vijana wetu wanaolalamika mitaani kuwa hawana
cha kufanya, tukiwajenga na kuwasimamia vijana wetu katika misingi ya
uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii umasikini utaondoka”
0 maoni:
Chapisha Maoni