Jumanne, 30 Agosti 2016

NDIKILO AKUTANA NA KAMATI YA AMANI KUZUNGUMZIA HALI YA KIUSALAMA MKOANI PWANI

Postedy by Esta Malibiche on August 30.2016 in News

ndi
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amesema wanaendelea na mapambano katika eneo la Vikindu na kuimarisha ulinzi wilayani Mkuranga kufuatia kutokea matukio ya uvunjifu wa amani ili kuzidi kufichua wahalifu.
Aidha amevitaka vyama vya  siasa mkoani humo,kuacha kufanya maandamano ikiwemo ya umoja wa kupinga udikteta(UKUTA)na chama kitakachobainika hatua kali zitachukuliwa.
Katika hatua nyingine mhandisi Ndikilo ,amewaomba viongozi wa dini wasichoke kuliombea taifa,kumuombea rais John Magufuli na viongozi wote ili waendelee kuwatumikia wananchi kwa maslahi mapana ya taifa.
Aliyasema hayo, wakati kamati ya amani ya mkoa wa Pwani,ilipokwenda kutoa pole kwa kamati ya ulinzi na usalama mkoani hapo ,kutokana na matukio ya kiuhalifu yaliyotokea wiki iliyopita wilayani Mkuranga.
Alisema kuwa serikali hiyo, imejipanga kikamilifu kulinda amani ya wananchi na mali zao sambamba na kuimarisha ulinzi wilayani ya Mkuranga na maeneo mengine ya mkoa.
“Tutahakikisha tunapambana na suala hili kwa kushirikiana na jeshi la polisi Dar es salaam na kwa kupitia uongozi wa amri Jeshi mkuu litakwisha kwani amedhamiria kwa dhati kupambana na jambo hili ,”
“Na askari hawajakatishwa tamaa ,licha ya kutokea kwa matukio hayo na kwasasa askari wengine bado wanaendelea na mapambano katika maeneo ya wilaya hiyo ili kufichua wahalifu wengine”alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo,alielezea kuwa,kuna kila sababu ya kuimarisha ulinzi na usalama ili hali wananchi waendelee kufanya shughuli zao kwa amani pasipo hofu.
Alisema dhamana ya kulinda amani ya watanzania ni ya serikali iliyopo madarakani na wakuu wa mikoa ni wasaidizi wa mh.rais na wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama hivyo atahakikisha anasimamia suala hilo .
Hata hivyo,mhandisi Ndikilo,aliitaka kamati ya amani mkoa,iendelee kushirikiana na serikali ngazi ya wilaya na kuangalia namna ya kuunda kamati hizo wilayani ili zishirikiane kuimarisha utulivu.
Akizunguzmzia kuhusiana na maandamano yanayotarajiwa kufanyika sept mosi mwaka huu,na umoja wa kupinga udikteta(UKUTA),alisema mkoani humo hayataruhusiwa .
Mhandisi Ndikilo,alieleza maandamano hayo hayana tija na mwisho wa siku ni kuleta vurugu na kuhatarisha amani ya mkoa na nchi kijumla hivyo utii wa sheria bila shuruti unahitajika.
Alisema ni vema vyama hivyo vikazingatia taratibu zilizowekwa na serikali ili kuepusha uvunjifu wa amani katika mkoa na endapo kipo chama kitakachokaidi taratibu zilizowekwa,hakitoweza kuvumiliwa.
Mhandisi Ndikilo,aliomba viongozi wa dini wayakataze kwa waumini wao kupitia misikiti na makanisa kwani yamepigwa marufuku.
“Haijakatazwa mikutano ya siasa bali wafanyie kwenye maeneo yao ya kazi kama ni mbunge ama diwani afanye kwenye eneo lake,sio diwani wa mailmoja aende Chalinze hapana,mtusaidie kufikisha salamu kuwa mkoa hautaki kusikia wala kuona maandamano ya UKUTA sijui nini”alisisitiza mkuu huyo.
Kwa upande wake ,kamanda wa polisi mkoani Pwani,kamanda Boniventure Mushongi ,alitoa rai kwa jamii kuendelea kutoa ushirikiano na jeshi la polisi kufichua wahalifu.
Alisema kwasasa wanaendelea na kulinda maeneo mbalimbali ya wilaya ya Mkuranga na kusema matukio mbalimbali yanatokea mara kwa mara wilayani humo, kutokana na maeneo mengi kuwa mapori ambapo baadhi ya watu wahalifu wamegeuza kuwa chocho na maficho yao.
Kamanda Mushongi ,alisema jeshi hilo halitosita kuingia kwenye mapori na maficho ambayo wananchi wasamaria wema watatoa taarifa kwa polisi kuyafanyia kazi.
Alisema kuwa ,kikulacho kinguoni mwako hivyo inapaswa jamii itambue hilo kwa manufaa ya mkoa na taifa kijumla.
Kamanda Mushongi,alieleza wananchi wajaribu kuwa macho ambapo aliwaomba watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kutoa mwiba unaosumbua.
Aliasa amani ilindwe na kila mmoja na ni jukumu la kila mmoja kuwa mlinzi wa mwingine na kushirikiana.Katika kamati ya amani mkoani hapo,ina wenyeviti wenza wawili,alhaj shekhe Hamis Mtupa na padre Beno Kakudo,ambao waliliomba jeshi la polisi lisikatishwe tamaa na yaliyotokea .
Alhaj Mtupa alisema,kweli polisi wengine wamepoteza maisha lakini wasikatishwe tamaa kwani polisi hao wamepotea maisha wakiwa kwenye mapambano na majukumu yao ya kazi.
Alihakikisha kuwa kwa nafasi zao kama viongozi wa kiroho wapo pamoja na wananchi na vyombo vya dola ambavyo vipo kwa ajili ya kulinda jamii na mali zao.
Alhaj Mtupa alisema viongozi wa kisiasa wajaribu kujenga tabia ya kupenda kukaa kwenye meza za mazungumzo ,kupatanisha na kujadili mambo kuliko kwenda katika hatua za maandamano,migogoro ama mapambano hali ambayo inawaweka wananchi katika hali ngumu.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama,alichukuwa fursa hiyo,kukemea maandamano hayo na kusema atakaekiuka taratibu zilizowekwa na serikali itageuka kichaka badala ya Ukuta.
Alisema Ukuta wanataka muafaka anashangaa hakuna tatizo ,watu wanafanya fujo halafu hao hao wanasema wanataka muafaka .
Assumpter alisema,wapo watu wanafanya mambo kwa kutaka kuvuruga amani ya nchi wakati nchi siyo ya kuichezea
Aliomba vijana na wananchi wilayani Kibaha,wawe watulivu siku ya sept mosi ili kuondokana na madhara yanayoweza kujitokeza.
Mnamo agost 26 mwaka huu mapigano makali yalitokea baina ya askari polisi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi huko eneo la Vikindu wilayani Mkuranga na kusababisha askari mmoja kufariki dunia na majambazi 14.
Agost 24 majira ya saa 1 /2 usiku ,uvamizi na shambulizi lenye nia ya uovu lililofanywa na kundi la majambazi na kuwauwa askari wanne huko Mbande huko Temeke,ambapo majambazi waliofanya tukio hilo wanadaiwa kuuwawa katika tukio la agost 26 eneo la Vikindu.

0 maoni:

Chapisha Maoni