Postedy by Esta Malibiche on August 28.2016 in News
Na Ismail Ngayonga-MAELEZO
Dar es Salaam
WAZIRI wa zamani wa mambo ya
ndani ya nchi, Augustino Mrema amewataka Watanzania kuyapuuza
maandamano ya Septemba Mosi mwaka huu yaliyoandaliwa na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na badala waendelee na shughuli za
ujenzi wa Taifa.
Mrema alisema hakuna haja ya
kufanya maandamano Septemba Mosi kwani hayana faida yoyote kwa taifa
badala yake wananchi wa kawaida ndio watakaoathirika.
Akizungumza katika mahojiano
maalum na mwandishi wa habari hii leo Jijini Dar es Salaam, Mhe. Mrema
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Misamaha kwa Wafungwa
(Parole) alisema mikutano ya hadhara na maandamano yasiyokwisha kila
kukicha yatasababisha wananchi wasifanye kazi.
Nchi yetu ni maskini hivyo
tunahitaji wananchi wafanye kazi kwa bidii” alisema Mrema. Alisema iwapo
CHADEMA wataona wameonewa ni vyema watumie njia za mazungumzo au
ikibidi kwenda mahakamani badala ya kufanya maandamano ambayo yanaweza
kusababisha vurugu na kuharibu amani na utulivu wa nchi.
Aliwataka Watanzania kukumbuka
maandamano ya mwaka 2001 yaliyoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) huko
Zanzibar ambapo watu kadhaa waliuwawa na mamia kukimbilia uhamishoni
nchini Kenya na Somalia.
Akizungumzia kuhusu utendaji
kazi wa Serikali ya Awamu, Mhe. Mrema alimpogeza Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kwa hatua yake ya kurejesha maadili na miiko ya utumishi kwa
watumishi wa umma nchini hali iliyosaidia kurejesha uwajibikaji wa
Serikali kwa wananchi.
Mrema alisema tangu kuingia
madarakani kwa Serikali ya Awamu Tano, kumekuwepo na mabadiliko kwa
watendaji wa umma katika ngazi mbalimbali za kimamlaka ukitofautisha na
miaka ya nyuma ambapo baadhi ya watendaji walikuwa wakifanya kazi kwa
mazoea.
“Viongozi wengi wa umma walikuwa
wakifanya kazi kwa mazoea bila kujali wajibu wao na wala hakukuwa na
uwajibikaji cha kusikitisha mamlaka husika zilikuwa haziwachukulii hatua
za kinidhamu, hivyo viongozi wa umma badala ya kuwatumikia wananchi
wakawa wanatumikia matumbo yao” alisema Mrema.
Mrema alisema Rais Magufuli
ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa kwa wananchi ya
kuwaondoa madarakani viongozi wazembe na wasiowajibika na wasiokuwa na
uwezo wa kufanya kazi katika kuwatumia wananchi.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu
ya Tano inastahili pongezi kwa hatua inazochukua katika mapambano dhidi
ya vitendo vya rushwa na ufisadi ikiwemo uanzishwaji wa Mahakama ya
Mafisadi nchini, kwani hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana katika
nchi pasipo na kupiga vita rushwa.
Mrema alisema ni wajibu wa kila
mwananchi kuichukia rushwa kwa vitendo ikiwemo kuwafichua hadharani
kikundi cha watu kinachojihusisha na rushwa kwani kwa kufanya hivyo
kutasaidia Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Kama mnavyokumbuka mimi
nilifukuzwa kazi serikalini kwa sababu ya kupinga ufisadi ambao kwa
wakati ule ulikuwa umekithiri serikali, ivyo nilichokuwa nikikipigania
mimi ndicho anachifanya Rais Magufuli” alisema Rais Magufuli.
Akizungumzia kuhusu hatua ya
Serikali ya Awamu ya Tano kuhamishia shughuli zake Mjini Dodoma, Mrema
alipongeza uamuzi huo kwani kiulinzi na kiusalama Dodoma ni pazuri zaidi
kuliko Dar es Saalam kwani ni katikati ya nchi.
“Dodoma panafaa sana kiulinzi na
usalama kwa kuwa ni vigumu kwa adui watoke baharini wafike hadi Dodoma
kabla hawajathibitiwa” alisema Mrema.
“Kuhusu ubora wa miundombinu ya
Mkoa wa Dodoma Mrema alisema Mkoa huo unafikika kirahisi zaidi kwa
wananchi waishio mikoa ya pembezoni na mipakani kufika Dodoma kuliko
ilivyo Dar es salaam ambayo iko Mashariki kabisa ya nchi” alisema
Mrema.
0 maoni:
Chapisha Maoni