Postedy by Esta Malibiche on August 25.2016 in KITAIFA
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa
inatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia mwezi ujao
baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliokuwa unajengwa.
Mradi huo unajengwa kwa usimamizi
wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Sumbawanga
(SUWASA), kwa ufadhili wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya
Ujerumani kupitia benki yake ya Maendeleo (KfW), sh. bilioni 31
utakapokamilika.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo
jana (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati na akiweka jiwe la msingi la
mradi wa maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Sumbawanga
na kuitaka kampuni ya kampuni ya Techno Fab Gammon Joint Venture ya
India kumaliza ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo.
Alisema mradi huo ambao tayari
umekamilika kwa asilimia 85 unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu,
hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanashirikiana na Manispaa katika
kulinda miundombinu ya mradi huo mara utakapokamilika pamoja na kutunza
vyanzo vya maji.
“Pamoja na Serikali kutumia fedha
nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji inayojengwa katika maeneo
mbalimbali nchini,changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa kubwa
kutokana na baadhi ya visima vimeanza kukauka hali inayosababishwa na
uharibifu wa mazingira,” alisema.
Alisema kumekuwa na uvamizi mkubwa
katika maeneo ya vyanzo vya maji ambapo wananchi wanajishughulisha na
shughuli za ulimaji, uchungaji wa mifugo, ujenzi wa nyumba za makazi na
uchomaji misitu hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira na hatimaye
vyanzo hivyo hukauka.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu
amewaagiza wakuu wote wa wilaya na wenyeviti wa vijiji nchini
kuyasimamia maeneo yenye vyanzo vya maji na kuwaondoa watu
wotewalioyavamia kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na
kuwafikisha mahakamani.
Naye Naibu Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe ambaye alimuwakilisha Waziri wa Maji
na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge katika hafla hiyo alisema
aliishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa nchi za Ulaya kwa
kufadhili mradi huo.
Hata hivyo Mhandisi Kamwelwe
alisema suala la kuhifadhi mazingira ni msingi endelevu wa upatikanaji
wa maji safi na salama, hivyo aliwaomba wananchi kujiepusha na uchafuzi
wa vyanzo vya maji na uharibifu wa mazingira ili kuepuka athari ya Taifa
kukubwa na janga la ukame.
“Wananchi wanatakiwa kuacha
kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kulima, kufuga ndani ya mita 60
kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji ili kuepusha
uharibifu wa mazingira ambao madhara yake ni makubwa kwa viumbe wote,”
alisema.
0 maoni:
Chapisha Maoni