Mchezaji maarufu wa mpira wa kikapu ambae kwasasa amestaafu mchezo huo Kobe Bryant ameanzisha mradi wa uwekezaji katika teknolojia, vyombo vya habari, na makampuni ya data wenye thamani ya dola milioni 100.
Bryant ameungana na mjasiriamali maarufu na mwekezaji katika Teknolojia Jeff Stibel ili kuzindua rasmi mradi huo jijini Los Angeles, mradi ambao hadi sasa wawili hao wamesema hauhitaji fedha za msaada ama ufadhili kutoka sehemu yoyote .
Wawili hao tayari wameshawekeza katika biashara takribani 15 wakiwa pamoja tangu mwaka 2013 ikiwa ni pamoja na tovuti maarufu ya michezo ijulikanayo kama ‘Players Tribune’, kampuni ya kutengeneza na kuuza program iitwayo ‘RingDNA’, kampuni ya kutengeneza mchezo wa video maarufu kwa jina la  ‘Scopely’ na nyinginezo.
BN-PM831_KOBE08_M_20160822133828
Kobe Bryant na Jeff Stibel katika uzinduzi wa mfuko wa mradi huo. (Picha na BRENDAN MCDERMID/REUTERS)
Stibel anafahamika  kama Mtendaji mkuu wa wa zamani wa kampuni ya umma ya teknolojia iitwayo ‘Web.com’ mbali na hayo ameanzisha na kufadhili makampuni ya kiteknolojia na biashara za masoko lakini pia ni mwanasayansi Bryant kwa upande mwingine anatarajiwa kutoa utaalamu wake wa ubunifu wa masoko ili kuongeza nguvu katika mradi huo.
Bryant na Stibel wanatarajia fedha hizo walizozitoa zitatosheleza katika mradi huo wa uwekezaji na utawaletea faida kutokana na ujuzi na uzoefu wa muda mrefu waliokua nao katika masuala ya uwekezaji, ujasiriamali, ubunifu wa kibiashara na ufahamu wa teknolojia.
Na Hashim Ibrahim (UDSM-SJMC)