Postedy by Esta Malibiche on August 25.2016 in KITAIFA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa
siku mbili kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi na Miundombinu wa mkoa wa Rukwa
pamoja na Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga kutatua matatizo ya
ardhi yanayowakabili wakazi wa Manispaa hiyo.
“Ijumaa kuanzia saa 3.00 asubuhi
wenye kero za ardhi wote waende kwenye ukumbi wa Manispaa mkuu wa idara
atakuwa na watumishi wote na hapa mtasikilizwa kero zenu na kupatiwa
ufumbuzi. Nasiku hiyo hakuna kazi nyingine ni kusikiliza wananchi tu,”
alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana
jioni (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na maelfu ya
wakazi Mji wa Sumbawanga waliojitokeza katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini
ambapo aliwasisitiza watendaji hao kuwasikiliza wananchi na kutatua kero
zao.
Alisema tangu alivyoanza ziara
yake katika mikoa ya Rukwa na Katavi kila eneo alilopita amekutana na
wananchi wakiwa na mabango yanaeleza changamoto na hii inatokana na
viongozi wa mikoa hiyo kushindwa kutenga siku maalumu kwa ajili ya
kusikiliza kero hizo.
Waziri Mkuu alibainisha kwamba
baadhi ya mikoa na halmashauri mbalimbali nchini zimeshaanza utaratibu
huo wa kutenga siku maalumu katika wiki na kusikiliza matatizo
yanayowakabili wananchi jambo ambalo limeanza kuonesha mafanikio ya
utatuzi wa kero hizo.
Awali akizungumza katika mkutano
huo mbunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hilaly alisema wakazi wa
Manispaa ya Sumbawanga wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya
migogoro mikubwa ya ardhi, hivyo alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia katika
kuipatia ufumbuzi.
Mbunge huyo alisema migogoro hiyo
ambayo imedumu kwa muda mrefu imewasababishia usumbufu mkubwa wakazi wa
jimbo hilo kukosa haki zao na muda mwingi wamekuwa wakiutumia
kufuatilia hatma ya ardhi yao bila ya mafanikio hivyo kurudi nyuma
kimaendeleo.
Pia mbunge huyo alimuomba Waziri
Mkuu kuwaondolea zuio la kuuza mazao yao nje ya nchi kwa sababu kitendo
hicho kimesababisha kushuka bei ya mahindi na kusababisha hasara kubwa
kwa wakulima ambao wametumia gharama kubwa katika kuandaa mashamba.
Akizungumzia zuio hilo Waziri Mkuu
alisema lengo la Serikali kuzuia uuzwaji wa mazao nje ni kutaka
kujiridhisha na uwepo wa chakula cha kutosha nchini ili kuepuka
kukumbwa na baa la njaa na kisha kwenda kuomba msaada kwenye nchi
tuliowauzia.
Kuhusu suala la soko la mahindi
Waziri Mkuu alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
watanunua kwa bei ya soko na kwamba wataruhusiwa kuuza nje ya nchi baada
ya Serikali kujaza maghala yake huku wataalam wakimalizia kufanya
tathmini ya hali ya chakula nchini.
0 maoni:
Chapisha Maoni