Postedy by Esta Malibiche on August 30.2016 with No comment
(Na Jovina Bujulu, MAELEZO)
Hivi karibuni
Serikali imetangaza kununua ndege nne katika kipindi cha mwaka huu wa
fedha kwa ajili ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ili kuimarisha
sekta ya usafiri wa anga hapa nchini zitakazogharimu Dola za Kimarekani
milioni 46.
Serikali kwa
kuanzia imetoa asilimia 40 ambazo ni sawa shilingi bilioni
39,937,939,200 kwa ajili ya ununuzi wa ndege mbili za awali .ambazo
zimelipwa Kampuni ya Bombadier Inc ya nchini Canada.
Azma hiyo ya
Serikali ya kununua ndege mpya inatokana na ahadi za Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kutaka kufufua
Shirika la Ndege Tanzania na kulipatia mtaji ili lianze upya kutoa
huduma hiyo kwa Watanzania.
Ujio wa ndege
hizo utaimarisha huduma za usafiri wa anga na kuongeza ushindani katika
utoaji wa huduma za anga hapa nchini kati yake na kampuni binafsi za
ndege zinazotoa huduma hiyo kwa sasa.
Mara baada ya
ndege hizo kuwasili hapa nchini zitaanza kutoa huduma ya usafiri wa anga
hapa nchini kabla ya kupanua wigo wake wa utoaji wa huduma katika ngazi
ya ukanda wa Afrika Mashariki na baadaye katika anga.nyingine za
Kimataifa.
Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame Mbarawa (MB)
aliwasilisha Bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha
hivi karibuni alisema kuwa Shirika la ATCL lina ndege moja aina ya Dash
8-Q300 na ndege ya kukodi aina ya CRJ 200.
“Kwa sasa ATCL
ina ndege moja na ndege nyingine ni ya kukodi ambazo zinawezeshwa na
Serikali kutoa huduma za usafiri wa anga kati ya Dar es salaam, Mwanza,
Mtwara, Kigoma na Moroni Comoro” alisema Profesa Mbarawa.
Aidha, Prof.
Mbarawa aliongeza kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na kampuni ya ATCL
na wadau wengine imekwishaainisha ndege mbili zinazofaa kununuliwa
ambazo zitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 78 na baadaye ndege nyingine
mbili kubwa zitakazokuwa na uwezo wa kubeba abiria 155 ambazo
zitanunuliwa kwa kipindi cha mwaka huo fedha.
Mchakato wa
ununuzi wa ndege hizo mbili ambazo zitanunuliwa katika awamu ya kwanza
ulihusisha wawakilishi wa viwanda vya ndege vya Boeing ya Marekani,
Airbus ya Ufaransa, Embraer ya Brazil na Bombadier ya Canada.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani alisema kuwa
ndege hizo ambazo zinatarajiwa kununuliwa zitatumia anga la Tanzania
ambapo hivi sasa anga hilo linatumiwa na ndege zinazotoka nje ya Afrika,
hivyo upatikanaji wa ndege hizo utasaidia kutoa fursa kutua kwenye anga
za nchi jirani.
“Muda si mrefu
tutapata ndege mbili mpya, mwakani tutaongeza nyingine mbili, Serikali
imejipanga kufufua Shirika la Ndege na kubadilisha mfumo wa uendeshaji
ili liweze kujiendesha lenyewe” alisema Mhandisi Ngonyani.
Kwa mujibu wa
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, (Mawasiliano)
William Budoya , amesema kuwa msukumo wa kununua ndege hizo ni jambo la
muda mrefu kuanzia Serikali ya Awamu wa Nne 2005-2015,na katika
kuendeleza utekelezaji wa juhudi hizo Serikali ya Awamu ya Tano imetoa
msisitizo na kulipa kipaumbele suala hilo.
Aidha, Afisa
Mawasiliano huyo amesema kuwa ndege zitakazonunuliwa ni aina ya
Bombadier kutoka kampuni ya Bombadier Inc ya nchini Canada.
Serikali
ilichagua kampuni ya Bombadier Inc kwa sababu iliainisha mchanganuo wa
biashara ambao ulishauri kuanza na ndege ndogo, kwa kuangalia soko la
ndani baadaye ndege zinaweza kuongezwa kwa kuangalia soko la kimataifa.
Aliongeza kwa
ndege hizo zinatarajia kufika nchini ifikapo mwezi Septemba mwaka huu,
na kwa kuanzia zitaanza kutoa huduma kwa safari za ndani ya nchi.
Aidha alisema
kuwa Serikali imemteua mshauri mwelekezi ambaye ataweka manejimenti
imara katika uendeshaji ikiwa ni pamoja na kuajiri wafanyakazi walio na
weledi na wenye utayari wa kufanya kazi kwa ufanisi.
Shirika la ndege
la Tanzania (ATC) lilianzishwa mwezi Machi, 1977 chini ya sheria ya
Mashirika ya Umma ya mwaka 1969 na baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa
Shirika la ndege la Afrika Mashariki.
Katika
kutekeleza sera ya ubinafsishaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi
katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ya mwaka 2002, Shirika la ndege
la Tanzania (ATC) liliundwa upya huku Serikali ikimiliki asilimia 49
ya hisa zake kwa Shirika la ndege la Afrika Kusini hatua ambayo
ilipelekea kuundwa upya kwa kampuni ya ndege Tanzania (ATCL).
Pamoja na kuwepo
kwa kampuni ya ndege ya ATCL, kwa sasa kuna kampuni binafsi
zinazojihusisha na huduma za usafiri wa anga nchini na nje ya
nchi.Kampuni hizo ni Precision Air, Fastjet, Auric na Coastal Air.
Akizungumzia
mpango wa Serikali wa kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa
zikiikabili kampuni ya ATCL , Budoya alisema kuwa mshauri mwelekezi
aliyeteuliwa na Serikali atatayarisha mpango madhubuti wa kibiashara
utakaoifanya kampuni ya ATCL kujiendesha kwa faida na kuweza kuteka soko
la ndani na nje ya nchi.
Majukumu ya
sekta ya uchukuzi yanasimamiwa Sera ya Taifa ya Uchukuzi ya mwaka (2003)
na utekelezaji wake ambao unahusu usafiri na usafirishaji kwa njia ya
anga, kusimamia viwanja vya ndege na usalama katika usafirishaji nchini.
0 maoni:
Chapisha Maoni