Postedy by Esta Malibiche on August 27.2016 in BIASHARA
Waziri Mkuu wa Japan ,Shinzo Abe
akizungumza katika mkutano wa Sita wa TICAD kwenye Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta jijini Nairobi Agosti 27, 2016.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa
Sita wa TICAD wakishiriki katika mkutano huo kwenye Kituo cha Mikutano
cha Kimataifa cha Jomo Kenyatta jijini Nairobi Agosti 27, 2016. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiw
katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wakuu wa Nchi na serikali
kwenye Kituo cha Mikutano cha Mikutano cha Jomo Kenyatta jijini
Nairobi Agosti 27, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka kwa nchi nyingine ambazo ni
wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani Afrika (APRM)
ili iweze kuboresha hatua ilizofikia kwenye mpango huo.
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Ijumaa, Agosti 26, 2016) wakati akichangia mada katika Mkutano wa 25 wa
Wakuu wa Nchi wanachama wa Mpango wa Kujitathmni Kiutawala Bora barani
Afrika (APRM Forum) uliofanyika kwenye hoteli ya InterContinental jijini
Nairobi, Kenya.
“Nitumie fursa hii kukiarifu kikao
chako kwamba Tanzania imeshaanza kutekeleza mpango kazi wa Kitaifa
ambao umejikita kutatua changamoto katika sekta za maji, elimu, kilimo,
nishati na miundombinu kama zilivyoainishwa kwenye kikao cha APRM,”
alisema.
“Ili kuhakikisha kuwa zinafanyiwa
kazi haraka, changamoto hizi za kisekta zimepewa kipaumbele kwenye
Mpango wetu wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano wa 2016-2021
ambao umejikita zaidi kwenye viwanda,” aliongeza.
Tanzania ilifanyiwa tathmini yake
Januari, 2013 kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika
kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia.
Mapema, akifungua mkutano huo,
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema viongozi wa Afrika hawana budi
kukubaliana na kuungana kutafuta suluhisho katika ushindani wa
kibiashara.
Alisema nchi wanachama wa mpango huo hawana budi kujenga umoja kama njia ya muafaka ya kufikia makubaliano hayo.
Wakati huohuo, Rais Yoweri
Museveni wa Uganda alisema bara la Afrika linakabiliwa na changamoto 11
(strategic bottlenecks) ambazo zinakwamisha maendeleo ya bara hilo na
akataka zitafutiwe ufumbuzi ili kuzisaidia nchi nyingi barani humo.
Akiwasilisha mada binafsi katika
mkutano huo, Rais Museveni alisema kwa zaidi ya miaka 50, amekuwa
kiongozi katika sehemu kadhaa na kwamba amebaini kuwa changamoto hizo
zimezuia ukuaji wa uchumi barani Afrika pamoja na mabadiliko ya kiuchumi
na kijamii.
Alisema asilimia kubwa ya
changamoto hizo haikupata ufumbuzi hata wakati malengo ya maendeleo ya
milenia (MDGs) yalipokuwa yanatekelezwa.
Alizitaja changamoto hizo kuwa ni
mikanganyiko ya kiitikadi ambayo huzaa ubinafsi na maslahi binafsi;
kuwepo kwa mataifa dhaifu (weak states); nguvukazi duni (kitaaluma na
kiafya), uduni wa miundombinu (barabara, maji, umeme, tehama) ambao
unashindwa kuvutia uwekezaji; uhaba wa viwanda unaolazimisha nchi
kusafirisha mali ghafi na uhaba wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa
barani Afrika.
Changamoto nyingine ni uduni wa
huduma za kijamii unaosababisha huduma mbovu kwenye maeneo ya utalii,
mabenki na mahoteli; kilimo duni kisichotumia mbolea, dawa za kuua
wadudu, mbegu za kisasa au njia za umwagiliaji; makosa ya kisera kama
vile ubinafishaji au utaifishaji mali zinazomilikiwa na sekta binafsi;
ukandamijazi wa demokrasia na ukosefu wa maadili miongoni mwa watumishi
wa umma.
Naye Rais Jacob Zuma wa Afrika
Kusini alisema kwa vile changamoto hizo zinagusa nchi nyingi za Afrika,
ni vema iundwe timu ya wataalamu watakazipitia zote na kuainisha zipi
zinafaa kufanyiwa kazi na kisha taarifa yao iwasilishwe kwenye kikao
kijacho cha Wakuu wa Nchi wanachama.
Akifunga mkutano huo, Rais
Kenyatta aliitaka sekretarieti ya APRM ipitie changaoto hizo na
kuziwakilisha kwenye kikao chao kijacho ambacho alisema kitafanyika
Januari 2017, mjini Addis Ababa, Ethiopia katika tarehe itakayopangwa
baadaye.
0 maoni:
Chapisha Maoni