Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU
wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amesema ni wakati wa kufanya
mabadiliko kwa kundi la vijana ,kwa kujenga tabia ya kujiajili wenyewe
,pasipo kutegemea kuajiliwa maofisini jambo ambalo linawachelewesha
kimaendeleo.
Aidha
ametoa rai kwa baadhi ya vijana kuacha kukaa vijiweni na kucheza pool
bali watumie fursa mbalimbali zinazowalenga ikiwemo kambi za vijana
,ujasiliamali na kilimo .
Aliyasema
hayo , wakati akizungumza na vijana waliopo kwenye kambi ya vijana
iliyopo Mkongo,wilayani Rufiji ambayo itahusisha vijana 200 kutoka
katika mikoa mbalimbali nchini,watakaopatiwa mafunzo ya kilimo maarifa
na ujasiriamali kwa vitendo .
Mhandisi Ndikilo
alisema vijana takribani bilioni 1.2 duniani hawana kazi ambapo
asilimia 80 wanatoka katika nchi za Afrika ikiwemo Tanzania hivyo
amezitaka mamlaka husika zinazosimamia mpango huo kuhakikisha kambi hiyo
siyo ya majaribio bali inakuwa endelevu.
Alisema
waendeshaji wa kambi hiyo wameanza vizuri kutekeleza agizo la Rais la
kutaka vijana kuondoka kwenye vijiwe na kuacha kuendekeza mchezo wa pool
.
“Kambi
hii ni sehemu ya kuwatayarisha kinadharia na vitendo kutekeleza dhana
nzima ya kuchangia katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya kilimo
nchini,hivyo ni vema mkaitumia vyema”alieleza Mhandisi Ndikilo.
Hata
hivyo ,mhandisi Ndikilo aliomba kusiwe na mzaha katika kusimamia
mpango huo na hataki kusikia unaishia kwa muda mfupi uwe endelevu.
Alieleza
kuwa amezindua kambi hiyo akitegemea kambi ya vijana ya Mkongo itakuwa
yenye tija na mfano ndani na nje ya Pwani na kwamba baada ya kuhitimu
wawafuatilie vijana huko watakapokuwa wanafanya kilimo .
Kaimu
mkurugenzi mkuu wa RUBADA dk. Deogratias Lwezaura alisema tayari awamu
ya kwanza ya mafunzo yameanza na vijana 62 kati yake 50 wametoka Rufiji
na watakuwa kambini kwa siku 10 .
Alisema
baada ya hapo watarudi kwenye mashamba yao na kuwafundisha wengine (
trainers of trainers ToTs) ambapo njia hiyo itasaidia kuondoa upungufu
wa maafisa wagani ndani na nje ya Rufiji.
Dk
Lwezaura alisema mpango wa mafunzo hayo kwa vijana utaendeshwa ndani ya
miezi 12 kuanzia mwezi huu na unalenga kuwajengea uwezo katika sekta ya
kilimo cha mbogamboga,ufugaji nyuki na wanyama ikiwa ni sanjali na
sungura na kuku.
Alitaja
changamoto zilizopo kambini kuwa ni uhakika wa maji safi ya kunywa na
kumwagilia mashambani kwani kwa sasa wanataumia ya kisima cha kijiji cha
Mkongo.
Dk.Lwezaura
aliiomba serikali isaidie kuvuta maji ya uhakika kutoka ziwa
Rungwe,tatizo jingine ni umeme uliopo ni wa nguvu ya jua kwa baadhi ya
nyumba hivyo wameomba kambi hiyo iingizwe katika mpango wa REA.
Nae
mkurugenzi wa SUGECO, Revocatus Kimario alieleza zipo shule nyingi
zinafundisha maarifa,sayansi,afya na mengine hivyo inahitajika elimu kwa
vitendo na uwezo wa kuunganisha maarifa hayo na uhalisia wake kwa
vitendo ili kujenga rasilimali watu na nguvu kazi iliyoelimika kwa
maarifa,ujuzi na uwezo na kutenda.
Alisema mpango wao ni kutoa elimu ya vitendo kwa asilimia 80 na maarifa ya darasani (soft skills) asilimia 20.
Awali
mwakilishi kutoka FAO ambao ndio wafadhili,Fred Kafeero alimweleza
Ndikilo kuwa katika programu hiyo watatengeneza miundombinu ya
umwagiliaji,umeme,vifaa na nyenzo za kufundishia .
Kafeero
alisema mpaka sasa wameshasaidia upatikanaji wa vifaa vya umwagiliaji
(drip irrigation) vyenye uwezo wa kumwagilia ekari tano la shamba la
mafunzo na wameajiri mratibu wa mafunzo na muhudumu wa ofisi .
Vijana
200 wanatarajiwa kunufaika katika mafunzo hayo ambapo pia mafunzo hayo
yanaendeshwa kwa ushirikiano wa mamlaka ya uendeshaji wa bonde la mto
Rufiji ( RUBADA), ushirika wa wajasiriamali wahitimu wa Chuo Kikuu cha
Sokoine (SUGECO) .
Wengine ni halmashauri ya wilaya ya Rufiji chini ya ufadhili wa shirika la chakula Duniani FAO kwa kipindi cha miaka minne.
0 maoni:
Chapisha Maoni