Postedy by Esta Malibiche on August 17.2016
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo wakati alipokuwa
akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Mkaramo kilichopo wilayani Pangani
mkoani Tanga (hawapo pichani)
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Mkaramo kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga. Waziri Muhongo yupo
mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya kusambaza umeme vijijini
inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na kuzungumza
na wananchi.
Wananchi wa kijiji cha Sakula
kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga wakionyesha mabango yenye
jumbe tofauti mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo (hayupo pichani) walipomsimamisha njiani kwa lengo la
kuwasilisha kero mbalimbali wakati akielekea katika kijiji cha Mkaramo
kwa ajili ya kuhutubia wananchi
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah Issa (kushoto) akiwasilisha mahitaji ya umeme katika wilaya ya Pangani
Waziri wa Nishati na Madini (kulia) akipokea kero mbalimbali kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mkaramo
………………………………………………………………………..
Na Greyson Mwase, Pangani
Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa Serikali ina mpango wa kusambaza
nishati ya umeme katika wilaya nzima ya Pangani na kuifanya kuwa wilaya
ya mfano ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Profesa Muhongo aliyasema hayo
alipokuwa akihutubia katika kijiji cha Mkaramo kilichopo wilayani
Pangani mkoani Tanga. Profesa Muhongo yupo mkoani Tanga kwa ajili ya
kukagua miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayotekelezwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kabla ya kuwasili katika kijiji
hicho msafara wa Profesa Muhongo ulisimamishwa na wananchi wa kijiji
cha Sakura kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga waliokuwa na
mabango wakiomba kupatiwa umeme katika kijiji chao.
Akizugumza kwa niaba ya wanakijiji
wenzake, Boga Mbega alisema kuwa kijiji hicho kimekuwa gizani kwa
muda wa miaka mingi hali inayopelekea uchumi katika kijiji hicho
kudumaa.
Aliongeza kuwa kutokana na ukosefu
wa umeme katika kijiji hicho wamekuwa wakifuata huduma za jamii kama
vile matibabu na maji katika vijiji vya mbali na hivyo kuhisi kama
wako kwenye kisiwa cha giza.
Mara baada ya Waziri Muhongo
kuwasili katika kijiji cha Mkaramo na kuanza kuhutubia alisema kuwa
kutokana na wilaya ya Pangani kuwa nyuma kimaendeleo kuliko wilaya
nyingine nchini, Serikali imepanga mikakati ya kuhakikisha kuwa wilaya
nzima ya Pangani pamoja na vijiji vyake vyote inapata nishati ya
umeme ndani ya kipindi cha miaka miwili.
Akielezea malengo ya kuipa
kipaumbele wilaya ya Pangani kwenye mpango wa usambazaji wa umeme
vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Profesa Muhongo
alieleza kuwa ni kufuta umasikini kupitia uboreshaji wa huduma za jamii
kama shule, zahanati, pamoja na kuzalisha ajira na kupunguza wimbi la
vijana kukimbilia mjini kutafuta ajira.
Alisema katika utekelezaji wa
mradi wa REA Awamu ya tatu katika wilaya ya Pangani, maeneo
yatakayopewa kipaumbele cha kwanza ni pamoja na shule, zahanati, vyuo,
makanisani na misikitini.
Aliwataka wananchi wa wilaya ya
Pangani kujiandaa na mradi huo kwa kubuni fursa mbalimbali kama vile
kuanzisha vikundi vidogo vidogo kwa ajili ya kuanzisha viwanda,
ukulima na ufugaji wa kisasa ili kujipatia maendeleo.
Alifafanua kuwa ni wakati wa wakinamama wa wilaya ya Pangani kuachana na matumizi ya kuni na kutumia majiko ya umeme na gesi.
Profesa Muhongo aliendelea kusema
kuwa miradi ya umeme haihitaji siasa na kuwataka wananchi kuweka nguvu
zaidi kwenye uchumi kwa kutumia nishati ya umeme badala ya kupoteza
muda kwenye siasa.
Naye Mbunge wa Pangani Jumaa
Hamidu Aweso (CCM) aliishukuru serikali kwa kuipa kipaumbele wilaya ya
Pangani na kusisitiza kuwa wataanza kufanya uhamasishaji kwa wananchi
wote wa Pangani .
Aliwataka wananchi kuachana na
maandamano ya siasa na badala yake waweke nguvu kwenye shughuli za
kiuchumi zitakazowapatia maendeleo.
Alisema kuwa mara baada ya umeme
katika wilaya nzima ya Pangani kupatikana, wawekezaji watajitokeza
kuwekeza kwenye viwanda vya korosho na kuongezeka mapato katika
halmashauri ya Pangani.
0 maoni:
Chapisha Maoni