Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
imeandaa operesheni kabambe katika stendi ya Mbagala ili kuhakikisha
biashara zote zinafanyika katika maeneo yaliyotengwa na yasiyohatarisha
afya ya jamii.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya
kuongezeka kwa malalamiko kutoka kwa wananchi wa eneo hilo juu ya
wafanyabiashara mbalimbali waliovamia eneo hilo na kulifanya kuwa la
biashara.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Nassib Mbaga na kuwataka
wafanyabiashara wanaofanya biashara zao katika mazingira yasiyo rasmi
kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria na taratibu.
“Tumeandaa operesheni kabambe ya
kuondoa Kero zilizogundulika katika stendi ya Mbagala ili kuhakikisha
kwamba biashara zote zinafanyika katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
shughuli hizo” alisema Mbaga.
Aliongeza kwa kuwataka watu wote
wanaofanya biashara bila kibali katika maeneo ya stendi hiyo waondoke
kabla ya zoezi la kusafisha halijaanza na kwa wale watakaokaidi, hatua
za kisheria zitachukulia dhidi yao.
Aidha Mbaga alieleza kuwa
kumekuwepo na jitihada za wazi za kuiweka Halmashauri katika hali ya
usafi ikiwemo kutoa elimu kwa umma pamoja na kuhamasisha wananchi kuweka
mazingira katika hali ya usafi na kuzuia unywaji wa maji ya kwenye
vifuko vya plastiki yajulikanayo kama viroba/Kandoro kwa kuwa hayana
viwango vya ubora.
Vilevile Halmashauri hiyo
itaendelea kuwakamata wale wote wanaofanya biashara hiyo na kuteketeza
mali zao kisha kuwafikisha Mahakamani au kuwalipisha faini.
Mkurugenzi huyo ameyataja maeneo
matano ambayo yametengwa rasmi kwa ajili ya biashara yakiwemo soko la
Toangoma, Kilamba, Makangarawe, Sigara na Kiponza ambapo maeneo hayo
yana huduma zote za jamii ikiwemo vyoo bora.
Maeneo mengine yaliyotengwa na
Halmashauri kwa ajili ya Masoko ni pamoja na Temeke Stereo, Vetenari
Tazara, Madenge, Tandika Kuu, Tandika Kampochea, Keko Magurumbasi,
Temeke Mwisho, Bulyaga, Kizuiani, Zakhem, Mbagala Rangi tatu, Kampochea
Mbagala, Mtoni Mtongani, Lumo, Urassa,Feri, Maguruwe, Limboa na Kabuma.
Mkurugenzi Mbaga ametoa rai kwa
wananchi wanaohitaji kupata nafasi za kufanyia biashara katika maeneo
mbalimbali ya Halmashauri hiyo kufanya mawasiliano na Ofisi yake ili
kupatiwa maeneo rasmi kwa ajili ya shughuli hizo
0 maoni:
Chapisha Maoni