Ijumaa, 19 Agosti 2016

WAAJIRI WATAKIWA KULINDA AFYA ZA WAFANYAKAZI

Postedy by Esta Malibiche on August 19.2016 in News

WHO -1
 Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi akizungumza wakati wa
mkutano wa wadau kuhusu usalama wa Afya mahali pa kazi jijini Dar es salaam.
1024×768
kiongozi wa Timu ya wataalamu wa Afya ya Jamii na Mazingira kutoka  Makao Makuu ya Shirika la Afya Duniani, Geneva,  Dk. Ivan Ivanov akizungumza wakati wa mkutano wa wadau kuhusu usalama wa Afya mahali pa kazi jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa – Dar es Salaam.
Waajiri kote nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao wa kisheria kwa wafanyakazi
waliowaajiri kwa kuhakikisha kuwa wanaweka mazingira mazuri ya kufanyia kazi na
kuwapatia vitendea kazi muhimu vya kuwakinga na madhara ya kiafya katika maeneo
yao ya kazi.
 Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau kuhusu usalama wa Afya mahali pa kazi jijini Dar es salaam, Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi amesema kuwa waajiri wana wajibu huo kwa kuwa maeneo ya kazi  ni sehemu muhimu katika maisha na uhai wa wafanyakazi kote nchini.
Amesema watumishi wamekuwa wakitumia muda mwingi kwa siku wakiwa mahali pa kazi kwenye viwanda, mashamba, maeneo ya kutolea huduma za Afya, migodini na kwenye
shughuli mbalimbali hivyo mazingira hayo lazima yawe salama kwa afya zao.
Ameongeza kuwa wafanyakazi katika maeneo mbalimbali nchini karibu kila siku wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zenye athari kwa afya zao hasa athari za kibiolojia, Kemikali, ajari za viungo vya miili yao, matatizo ya usikivu yanayotokana na mazingira yenye kelele na changamoto mbalimbali ambazo wakati mwingine husababisha vifo.
“Wapo baadhi ya waajiri hawatimizi wajibu wao wa kisheria wa kuhakikisha wanalinda afya za watumishi wao kwa kuwawekea mazingira safi na salama, jambo hili halikubaliki”
Amesisitiza Prof. Mohammed.
Amesema Serikali kupitia wizara ya Afya ikishirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya
Afya itaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali  zinazowakabili wafanyakazi katika sehemu zao za kazi kazi ili kulinda afya zao.
Kwa upande wake kiongozi wa Timu ya wataalamu wa Afya ya Jamii na Mazingira kutoka  Makao Makuu ya Shirika la Afya Duniani, Geneva,  Dk. Ivan Ivanov  amesema kuwa Tanzania ina wafanyakazi zaidi ya milioni 16 , wengi wao wakiwa kwenye sekta isiyo rasmi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa na chanzo cha kipato kwa jamii na Taifa.
Amesema utafiti uliofanywa na mtaalamu aliyeteuliwa na WHO umebainisha changamoto
mbalimbali ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na Serikali ili kuboresha maslahi na mazingira ya kufanyia kazi kwa kundi hilo.
“Ninajua wafanyakazi nchini Tanzania wamekuwa chanzo cha mapato, uzalishaji na ni
tegemeo kwa jamii na Taifa, wanapougua au kupata ajali kwa sababu ya mazingira
yasiyo salama hasara kwao wenyewe na kwa Taifa kwa kuwa hali hii inaongeza idadi ya wafanyakazi wagonjwa” Amesema Dk. Ivanon.
Amesema WHO inaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuweka msisitizo katika
kuboresha mazingira ya wafanyakazi katika sekta zote ili kudhibiti mazingira yenye viashiria hatarishi kwa afya za wafanyakazi maeneo ya viwanda, Sekta ya Afya, migodini na mashambani.
Amesema kuwa mchango wa WHO ikishirikiana na Tanzania ni kuboresha Mpango mkakati kwa
ajiri utakaowezesha uboreshaji wa Afya za wafanyakazi kuanzia ngazi ya ngazi ya kijiji hadi Taifa ili kuwalinda wafanyakazi wanaofanya kazi kwenye mazingira hatarishi kwenye sekta isiyo rasmi wakiwemo watoto na wazee.  
Amesema kufanyika kwa utafiti huo kunatokana na Azimio la mkutano wa Afya wa dunia
(World Health Assembly) lililotoka mwaka 2007 ambao ulizitaka nchi zote zitengeneze mpango wa utekelezaji kuhusu masuala ya Afya kazini.
Amesema kupitia Azimio hilo Tanzania ilianza kufanya utafiti mwaka 2005 na ripoti ya
utafiti huo imekamilika tayari kwa majadiliano yanayowahusisha wadau ili waweze
kutoka na mkakati wa utekelezaji wa kukabiliana na changamoto za afya kazini.
“Mwaka 2005 utafiti huu ulianza kufanyika sasa umekamilika, kwenye mkutano huo
wameitwa wadau ili kupata taarifa hii, kuijadili na kutoka na mkakati wa pamoja
wa kukabiliana na changamoto zote za masuala ya Afya Kazini” Amesema.
Amesisitiza kuwa suala la Afya kazini ni mtambuka kwa kuwa linahusisha wadau mbalimbali
pamoja na changamoto mbalimbali ikiwemo ufanyaji wa kazi katika mazingira yasiyo salama.

0 maoni:

Chapisha Maoni