Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) umepanga kufanya maandamano nchi nzima tarehe 30 Agosti, 2016 kwa namna yoyote ile, iwe kwa ruhusa ya Jeshi la Polisi ama kutoruhusiwa na jeshi hilo.
Uamuzi huo umetangazwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu UVCCM, Shaka Hamdu Shaka.
“Tarehe 31 Agosti, 2016 UVCCM tutaitisha maandamano ya amani nchi nzima, wakati Chadema wakitarajia kuitisha maandamano yasiyo na ukomo nchi nzima kuanzia septemba mosi mwaka huu, sisi tumepanga maandamano ya amani yenye lengo la kumpongeza rais,” amesema na kuongeza.
“Kwa dhamira yake ya wazi iliyokusudia kupambana na vitendo vya ufisadi, wizi, na ufujaji wa mali za umma,” amesema.
Amesema wanaandama katika mikoa yote ili kuuhakikishia ulimwengu kuwa wako bega kwa bega na wanamuunga mkono Rais John Magufuli.
“Ikitokea polisi hawatakubali kuyaruhusu maandamano hayo, UVCCM tutalazimika kuandamana kwa kujilinda wenyewe,” amesema.
Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,Simon Sirro amedai kuwa hawezi kuzungumzia suala lolote juu ya maandamano hayo kwa kuwa hana taarifa rasmi za maandamano kutoka kwa UVCCM.
“Siwezi nikazungumzia maandamano ya UVCCM kwa sababu sina barua wala taarifa rasmi inayosema kuwa umoja huo unahitaji kufanya maandamano,” amesema Sirro leo baada ya waandishi wa habari kutaka kujua msimamo wake juu ya maandamano hayo ya UVCCM.
Na Regina Mkonde