Katibu Mtendaji wa Baraza la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Benga’i Issa wa kwanza kulia
akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu maonesho ya
wajasiriamali yataofanyika Septemba 26 mwaka huu jijini Dar es salaam ,
kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini
(TPSF) Bw. Godfrey Simbeye.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi nchini (TPSF) Bw. Godfrey Simbeye kushoto akiongea na
waandishi wa habari hawapo pichani kuhusu maonesho ya wajasiriamali
yataofanyika Septemba 26 mwaka huu jijini Dar es salaam, kulia ni Katibu
Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Benga’i
Issa.
Picha Zote Na Ally Daud-Maelezo
………………………………………………………………
Na Ally Daud-Maelezo
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama anatarajiwa kufungua
maonesho ya wajasiliamali yatofanyika Septemba 26 katika viwanja vya
Mlimani City ambayo yameandaliwa na Taasisi ya Ujasiriamali na ushindani
Tanzania(TEEC) kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi (NEEC) pamoja na Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) ili
kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam Katibu Mtendaji wa NEEC Bi. Beng’i Issa
amesema kuwa maonesho hayo yatalenga kuwawezesha wananchi kuwa wabunifu
katika sekta ya biashara ili kupiga hatua kufikia uchumi wa kati.
“Maonesho ambayo yatafanyika kesho
ni kwa ajili ya wajasiriamali wote wakubwa, wa kati na wadogo ili
kuwawezesha kiujuzi na kiushindani katika soko la biashara” alisema Bi.
Issa.
Aidha Bi. Issa amesema kuwa siku
hiyo kutakuwa na kliniki ya biashara kwa watu wote kutoka kwa wataalamu
wa biashara ili kuweza kuwapatia mafunzo wajasiriamali wakubwa na wadogo
ili waweze kupata mafanikio yao na jamii kwa ujumla kupitia biashara
zao.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji
wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) Bw. Godfrey Simbeye amesema
kuwa maonesho hayo yatawajengea wajasiriamali fursa za masoko kwa
biashara nchini na Afrika kwa ujumla.
“kupitia maonesho hayo
wajasiriamali watapata fursa ya kutengeneza masoko ya biashara zao kwa
ubora zaidi nchini na afrika kwa ujumla ili waweze kujitangaza
kimataifa” alisema Bw. Simbeye.
Aidha Bw. Simbeye amesema kuwa
wana mpango wa kuwaelimisha wajasiriamali kwa wingi zaidi ili waweze
kuwa wabunifu na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya biashara ndani
na nje ya Tanzania.
Mbali na hayo Mkurugenzi Simbeye
amesema kuwa anawakaribisha watu wote wajasiriamali wakubwa na wadogo
kufika katika maonesho hayo ambayo hayana kiingilio ili waweze kupata
ujuzi wa kutosha kwa maendeleo ya biashara zao na kuinua uchumi wa nchi.
0 maoni:
Chapisha Maoni