Postedy by Esta Malibiche on August 20.2016 in News
Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
Dar es Salaam
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa kwa hatua yake ya
kurejesha maadili na miiko ya utumishi kwa watumishi wa umma nchini hali
iliyosaidia kurejesha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo Jijini Dar
es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi ya Misamaha kwa Wafungwa (PAROLE) na
Mbunge wa Zamani wa Jimbo la Vunjo, Mhe. Augustino Mrema wakati wa
mahojiano yake maalum na mwandishi wa habari hii akieleza kuhusu
mafanikio ya mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Tano
ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Mrema alisema tangu kuingia
madarakani kwa Serikali ya Awamu Tano, kumekuwepo na mabadiliko kwa
watendaji wa umma katika ngazi mbalimbali za kimamlaka ukitofautisha na
miaka ya nyuma ambapo baadhi ya watendaji walikuwa wakifanya kazi kwa
mazoea.
“Viongozi wengi wa umma walikuwa
wakifanya kazi kwa mazoea bila kujali wajibu wao na wala hakukuwa na
uwajibikaji cha kusikitisha mamlaka husika zilikuwa haziwachukulii hatua
za kinidhamu, hivyo viongozi wa umma badala ya kuwatumikia wananchi
wakawa wanatumikia matumbo yao” alisema Mrema.
Kwa mujibu wa Mrema alisema Rais
Magufuli ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa kwa
wananchi ya kuwaondoa madarakani viongozi wazembe na wasiowajibika na
wasiokuwa na uwezo wa kufanya kazi katika kuwatumia wananchi.
Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu
ya Tano inastahili pongezi kwa hatua inazochukua katika mapambano dhidi
ya vitendo vya rushwa na ufisadi ikiwemo uanzishwaji wa Mahakama ya
Mafisadi nchini, kwani hakuna maendeleo yatakayoweza kupatikana katika
nchi pasipo na kupiga vita rushwa.
Mrema alisema ni wajibu wa kila
mwananchi kuichukia rushwa kwa vitendo ikiwemo kuwafichua hadharani
kikundi cha watu kinachojihusisha na rushwa kwani kwa kufanya hivyo
kutasaidia Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo.
“Kama mnavyokumbuka mimi
nilifukuzwa kazi serikalini kwa sababu ya kupinga ufisadi ambao kwa
wakati ule ulikuwa umekithiri serikali, ivyo nilichokuwa nikikipigania
mimi ndicho anachifanya Rais Magufuli” alisema Rais Magufuli.
Wakati huo huo , Mhe. Mrema
amesema kuwa hakuna haja ya kufanya maandamano Septemba Mosi kwani
hayana faida yoyote kwa taifa badala yake wananchi wa kawaida ndio
watakaoathirika.
Amewasihi wananchi kutumia muda
huo kufanya shughuli nyingine za maendeleo badala ya kuandamana kwa
kuwa hakuna demokrasia isiyo na mipaka.
“Mikutano ya hadhara na
maandamano yasiyokwisha kila kukicha yatasababisha wananchi wasifanye
kazi. Nchi yetu ni maskini hivyo tunahitaji wananchi wafanye kazi kwa
bidii” alisema Mrema.
Aliwataka Watanzania kukumbuka
maandamano ya mwaka 2001 yaliyoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) huko
Zanzibar ambapo watu kadhaa waliuwawa na mamia kukimbilia uhamishoni
nchini Kenya na Somalia.
Akifafanua zaidi Mrema alisema
kuwa iwapo CHADEMA wataona wameonewa ni vyema watumie njia za
mazungumzo au ikibidi kwenda mahakamani badala ya kufanya maandamano
ambayo yanaweza kusababisha vurugu na kuharibu amani na utulivu wa nchi.
SERIKALI KUHAMIA DODOMA.
Akizungumzia kuhusu hatua ya
Serikali ya Awamu ya Tano kuhamishia shughuli zake Mjini Dodoma, Mrema
alipongeza uamuzi huo kwani kiulinzi na kiusalama Dodoma ni pazuri zaidi
kuliko Dar es Saalam kwani ni katikati ya nchi.
“Dodoma panafaa sana kiulinzi na
usalama kwa kuwa ni vigumu kwa adui watoke baharini wafike hadi Dodoma
kabla hawajathibitiwa” alisema Mrema.
“Kuhusu ubora wa miundombinu ya
Mkoa wa Dodoma Mrema alisema Mkoa huo unafikika kirahisi zaidi kwa
wananchi waishio mikoa ya pembezoni na mipakani kufika Dodoma kuliko
ilivyo Dar es salaam ambayo iko Mashariki kabisa ya nchi” alisema
Mrema.
0 maoni:
Chapisha Maoni