Postedy by Esta Malibiche on August 19.2016
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo kuhusu uboreshwaji wa
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT),kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho
Prof. Zacharia Mganilwa alipokagua chuo hicho jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, akikagua moja ya darasa linalotumika
kufundishia Marubani wa ndege alipokagua Chuo cha Taifa cha
Usafirishaji (NIT), jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na wanafunzi wanaosoma kozi
ya udereva alipotembelea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), jijini
Dar es Salaam. Kushoto (mwenye tai nyekundu) ni Mkuu wa Chuo hicho Prof.
Zacharia Mganilwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akibadilishana uzoefu na makapteni wa
meli ya Azam aliposafiri na boti hiyo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na mmoja wa abiria wanaotumia
usafiri wa boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, na kujionea
changamoto mbalimbali zinazowakabili abiria hao ambapo ameahidi
kuzipatia ufumbuzi hivi karibuni.
…………………………………………………………………………….
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali imejidhatiti
kufanya maboresho makubwa ya kimiundombinu na rasilimali watu katika
sekta za uchukuzi ili kuiwezesha sekta hiyo kuongeza ajira na kukuza
uchumi wa nchi.
Prof. Mbarawa amesema hayo mara
baada ya kukagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na kusafiri wa
boti kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ikiwa ni mkakati wa kupata
taarifa sahihi kuhusu hali ilivyo sasa kutoka kwa abiria na waendeshaji
wa vyombo vya majini.
Amesema Serikali itaboresha
Bandari ya Dar es Salaam ili kupunguza urasimu usio wa lazima na
kuwawezesha abiria na boti kukaguliwa kwa haraka na kuondoka kwa muda
unaotakiwa.
‘Tutahakikisha kuwa idadi ya
manahodha na wahandisi wa vyombo vya majini wazalendo inaongezeka ili
mkakati wa kuboresha usafiri wa majini hapa nchini uwiane na uwepo wa
wataalam wa uhakika’ amesema Prof. Mbarawa.
Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano amesema Serikali ina mpango wa kujenga meli mpya za kisasa
katika Ziwa Victoria ili kuhamasisha wasafirishaji katika sekta ya
usafiri majini kuwa na vyombo vya kisasa na hivyo kupunguza gharama za
usafiri.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amekagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ambapo
amesisitiza kuwa Serikali itaunga mkono juhudi zinazofanywa na Chuo
hicho katika kutoa mafunzo wa marubani wa ndege ili kuongeza idadi ya
marubani wazalendo.
‘Mpango wetu wakukunua ndege mpya
unaendana na kuwezesha Chuo hiki chenye kufundisha marubani ili tuwe na
marubani wazalendo wa kutosha’ amesisitiza Prof. Mbarawa.
Amewataka wafanyakazi wa Chuo
hicho kufanya kazi kwa uzalendo, ubunifu na kuzingatia matokeo ili
kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayokwenda haraka.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Profesa
Zacharia Mganilwa amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa chuo hicho
kitashirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mamlaka ya Reli ya
Tanzania na Zambia (TAZARA), Kampuni hodi ya Rasilimali za Reli (RAHCO)
katika kupata utaalam wa kisayansi katika mradi wa ujenzi wa reli ya
kati ya Kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Serikali imejipanga kujenga chuo
cha kisasa cha Usafirishaji kwa kushirikiana na Jamhuri ya Watu wa China
ikiwa ni mkakati wa kukifanya chuo hicho kuwa chuo mahiri katika upande
wa Afrika Mashariki na Kati.
Zaidi ya Shilingi trilioni 4
zimetengwa na Serikali katika bajeti ya mwaka huu ili kuimarisha
miundombinu ya usafiri wa Angani, barabarani, relini na majini.
0 maoni:
Chapisha Maoni