Postedy by Esta Malibiche on August 29.2016 in SIASA
Umoja
wa Vijana wa CCM tuliutangazia umma na dunia kwamba ifikapo Agosti 31
mwaka huu tutaitisha maandamano ya amani nchi nzima yenye lengo la
kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk
John Pombe Magufuli kwa utendaji wenye tija, ufanisi na uliorudisha
imani na matumaini kwa wananchi.
Msimamo na dhamira ya kufanya
maandamano hayo ya amani yenye maudhui na kusudio hilo, bado uko pale
pale ingawaje si kwa tarehe tuliopanga na kutangaza awali yaani Agosti
31 mwaka huu.
Jumuiya yetu kama mjuavyo ni ya Vijana
wa CCM, (UVCCM) inapata malezi kwa karibu mno na Jumuiya ya Wazazi ya
CCM. Wiki ya jana Mwenyekiti wa Wazazi Taifa Nd. Abdallah Bulembo
alikutana na waandishi wa habari akitutaka UVCCM tuahirishe maandamano
ya Agosti 31 mwaka huu hadi wakati mwingine.
Kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha
Mapinduzi, Jumuiya ya Wazazi ndiyo Msimamizi wa Malezi, Maadili na Adabu
kwa Vijana wote nchini, sisi UVCCM tunaamini kuwa sikio halishindani na
kichwa, mtoto ni mtoto kwa Wazazi wake hakui, hana jeuri wala ubishi.
Mtoto au watoto wanaokaidi amri,
ushauri au maelekezo ya Wazazi wao huitwa watukutu, wenye viburi,
manunda na wasioambilika. UVCCM si watukutu, hatukufunzwa tuwe wabishi,
wakaidi na wenye viburi. Tumezingatia kutii maelekezo, makatazo na
maonyo , tumeambiwa tuahirishe maandamano yetu nasi tumekubali na
kuheshimu mambo tuliyoaswa.
Sambamba na hilo tumepata majibu ya
barua yetu tuliyomwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP Ernes
Mangu) inayotutaka tuache kufanya maandamano yetu kwa sababu Polisi
wamezuia mikutano ya hadhara ya Vyama vya Siasa na maandamano nchi
nzima.
Jambo jingine ambalo limetufanya pia
tuahirishe maandamano yetu ya Amani ni taarifa ya kintelejinsia
iliowasilishwa na Kamati yetu ya Usalama na Maadili ya UVCCM mbele ya
kikao cha Sekreteriet yetu, nayo ilipendekeza suala hilo liahirishwe
kwa wakati huu hadi muda mwingine.
Pia jambo jingine ambalo limefanya
maandamano hayo tuyabatilishe ni kulipisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ ) ambalo litakuwa katika shughuli za maadhimisho miaka 52 tokea
kuanzishwa kwake.
Wanajeshi wetu watakuwa katika kazi
mbalimbali za kijeshi kwenye kambi zao na mitaani kufanya usafi wa
mazingira, hivyo isingependeza na wala si heshima wakati sisi
tukiandamana, wao wakifanya kazi muhimu kila mmoja wetu zinazomgusa
badala yake ni vyema kuwaunga mkono jambo wanalolifanya la usafi wa
mazingira.
UVCCM tumekubali, hatutaki kuingia
katika uvunjaji wa sheria hasa baaada ya kutakiwa kuahirisha na mamlaka
za Kisheria hadi wakati mwingine muafaka na si wakati huu.
Tunaelewa kwamba uamuzi wetu wa awali
wa kutaka kuandamana kwa amani hata kama tungenyimwa kibali
ungetugharimu, ungetusababishia madhara na pengine hasara, kwa wakati
huu na kuona jambo lenyewe ni la kuipa Ari serikali katika kuhimiza
Uwajibikaji, Utendaji na Usimamizi bora wa Uendeshaji wa masuala ya
kiutawala.
Tulishusha maagizo kwa Makatibu wetu
wote wa Mikoa yote 32 na Wilaya 171 ya Kichama tukiwataka waandike barua
katika Ofisi za Ma RPC na OCD, washirikiane ili kuratibu maandamano na
kuyafanikisha kama tulivyokusudia.
Watendaji wetu wa ngazi husika
wamefuata maelekezo, wametii taratibu zetu za kiutendaji na leo
tumewajulisha tena wasitishe maandamano hadi tutakapowapa tena maelekezo
mengine. Tunawahimiza na kuwataka ni vyema kutii mamlaka za Kikanuni na
Kisheria.
UVCCM kwa wakati huu tumeamua kuachana
na maandamano badala yake tunajikita katika matayarisho ya kuwapeleka
Vijana wetu wakashiriki katika Mafunzo ya Siasa, Utawala, Uongozi,
Ufundi na Ujasiriamali yatakayoanza kufanyika katika Chuo chetu
kilichopo huko Ihemi Mkoani Iringa ambapo kitakuwa kielelezo na alama
nzuri ya kumuunga mkono Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa vitendo.
Tumewataka Makatibu wetu wa Mikoa na
Wilaya kuendelea na zoezi la Uratibu na Uhakiki kwa Vijana ambao
watateuliwa kushiriki Mafunzo hayo huko Ihemi.
UVCCM tunarejea kusema tena kwamba
dhamira ya maandamano yetu ya kusifu Utendaji wa Serikali ya awamu ya
tano iko pale pale ila tutapanga tarehe nyingine katika wakati ujao
badala ya kufanyika Agosti 31 mwaka huu kama tulivyotangaza hapo awali.
UVCCM tunawataka Vijana wote kuendelea kuheshimu Tunu ya Amani Umoja na Mshikamo wetu kwa Taifa.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
0 maoni:
Chapisha Maoni